Monday, 12 August 2013

Samaki wa Idd aua watoto wanne

WATOTO wanne wa familia moja wamekufa kwa kula chakula kinachosadikiwa kuwa na sumu katika sikukuu ya Idd. Tukio hilo lilitokea Agosti 9, mwaka huu, katika kijiji cha Ligunga, kata ya Lusewa, wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, ambapo wanafamilia wengine 12 nao wamelazwa hospitali baada ya kuathiriwa na chakula hicho. Katibu Tarafa ya Sasawala, Fred Maliyao, aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa wanafamilia hao 16 walikula vyakula vya aina tofauti siku hiyo ambapo kimojawapo kinasadikiwa kuwa na sumu. Alivitaja vyakula hivyo kuwa ni ugali, samaki mbonga za majani, mbaazi na utumbo wa kuku. Akifafanua zaidi, mmoja wa wanafamilia, Bilahi Mumba aliwataja watoto waliokufa kuwa ni Zidane Mumba mwenye miaka miwili na nusu, Tazamio Mumba (9), Seleman Mumba (7) na Zahara Mumba (2). Alisema kuwa tukio hilo lilitokea kati ya saa 5:00 na 6:00 mchana baada ya watoto hao kula samaki kwa baba yao mdogo ambao aliwanunua katika eneo la Lusewa. Muuguzi wa kituo cha afya cha Lusewa, Edrisa Ndauka alikiri kuwapokea waathirika hao 16 ambapo wanne walifariki na watano walikimbizwa hospitali ya mkoa mjini Songea. Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Abdula Lutavi, ambaye alifika eneo la tukio, alisema tatizo hilo ni kubwa kutokana na waliokufa kuwa watoto wa familia moja. Alisema kuwa baada ya watalamu kupima matapishi na mabaki ya vyakula hivyo, taarifa ya awali ilionyesha kuwa sumu ilikuwa kwenye samaki kwani wote waliogusa kitoweo hicho au kunywa mchuzi wake walipata madhara. Aliwaonya wananchi kuacha tabia ya kuvua samaki kwa kutumia sumu ili kujiepesha na madhara kama hayo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Deusdedit Nsimeki, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanamshikilia mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Salum kwa mahojiano zaidi.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment