Sunday, 11 August 2013

Sheikh Ponda azua taharuki,waumini wadai kapigwa risasi na Polisi hawana taarifa hiyo!!!!!


TAHARUKI kubwa imezuka jana baada ya taarifa mbalimbali kuzagaa kuwa Katibu wa Taasisi na Jumuiya ya Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda, amepigwa risasi wakati akitoka katika mhadhara uliofanyika katika viwanja vilivyo karibu na Msikiti wa Dini Moja Mungu Mmoja mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali zilizozagaa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya watu waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili, zilisema kuwa tukio hilo lilitokea wakati kiongozi huyo alipoambatana na wafuasi wake wakielekea katika swala ya magharibi ndipo alipozungukwa na magari matatu ya polisi na kutaka kuondoka naye.
Taarifa hizo zilidai kuwa kiongozi huyo hakuwa tayari kutekeleza amri ya kuondoka na askari hao ndipo walipolazimika kutumia nguvu na kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya wafuasi hao.
“Tukio limetokea kweli na kulikuwa na matumizi ya nguvu ikiwemo mabomu ya machozi na ufyatuaji wa risasi kutoka kwa askari polisi lakini mhadhara wake haukuwa na fujo yoyote,” walisema watoa taarifa hao.
Kwa mujibu wa taarifa zilizozagaa zilisema kuwa polisi walifyatua risasi zilizompata kiongozi huyo begani lakini wafuasi wake walifanikiwa kumtorosha.

Zilisema kuwa kiongozi huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa kutumia usafiri wa pikipiki huku akiingizwa kwa kutumia geti la nyuma la hospitali hiyo.
Hata hivyo taarifa hizo zilisema kuwa Sheikh Ponda aliondolewa muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo na kukimbizwa kusikojulikana.
Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alisema kuwa taarifa nyingi zimeenea lakini wao kama Jeshi la Polisi hawana taarifa za kiongozi huyo kupigwa risasi.
Shilogile alisema kuwa polisi walikwenda kumfuata wakati gari lake likiwa linasukumwa kutokana na kutafutwa.
“Wakati wanamfuata pale polisi walilazimika kutumia risasi baridi ndipo wafuasi wake wakafanikiwa kumtorosha kwa pikipiki,” alisema kamanda huyo.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment