Shule zote za msingi katika Kijiji cha Bwilingu (Chalinze Mjini), kata ya Bwilingu Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, ziko katika hali mbaya kutokana na wanafunzi wake kusoma wakiwa wamekaa chini na katika msongamano mkubwa madarasani.
Pia, shule hizo zina uhaba mkubwa wa vyoo, hali inayowalazimu walimu wa kike na kiume kutumia tundu moja la choo cha wanafunzi na kukosekana kwa nyumba, samani na ofisi za walimu.
Katika Shule ya Msingi Chalinze Mzee, Mwalimu Mkuu kakosa ofisi na sasa kageuza choo cha wanafunzi wa kiume ambacho hakijaanza kutumika kama ofisi.
NIPASHE ilitembelea shule za msingi katika kijiji hicho na kubaini kuwa wanafunzi wanasoma kwa kupokezana kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa na kwenda chooni kwa kupanga foleni kutokana na uhaba wa vyoo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bwilingu, Ally Fani, akizungumza na NIPASHE mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema shule zote za msingi katika kijiji hicho zipo kwenye hali mbaya na hakuna fedha kwa ajili ya kukabiliana na matatizo hayo.
“Tunatafuta mfadhili wa kutusaidia kukabiliana na changamoto za uhaba wa nyumba vya madarasa, nyumba na ofisi za walimu, vyoo na madawati,”alifafanua.
Alisema shule ya msingi Chalinze Mzee ilianza mwaka 1999 kwa nguvu za wananchi na aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo, Nicodemas Banduka lakini baada ya hapo hakukuwa na ukarabati wowote uliofanyika.
Alisema choo kipya kilichopo kimejengwa kwa ufadhili wa wa Taasisi ya Ebenezer Spritual Center ya mjini Chalinze kimegharimu kiasi cha Sh. milioni 70.
Alisema serikali ya kijiji ina taarifa na hali mbaya katika shule hiyo na kwamba suala la Mwalimu Mkuu wa shule kuhamishia ofisi yake kwenye choo kipya kinachojengwa hawana taarifa nazo.
Alisema kamati ya huduma za jamii ya kijiji hicho ilitembelea shule hiyo mwaka jana na kuweka mikakati ya kuikarabati, kwa kijiji kutenga Sh. 600,000.
Mtendaji wa Kijiji hicho, Peter Ikanga, alisema matatizo yaliyopo kwenye shule hiyo na shule nyingine za kijiji yanajulikana na walishaiandikia Halmashauri ya wilaya juu ya shule hilo barua mbili kwa nyakati tofauti.
Alisema shule ya msingi Chalinze Mzee ilitembelewa na Kamati ya Wilaya mwaka jana na kujionea matatizo yaliyopo na kuweka mikakati ya kukabiliana nayo.
Mwenyekiti wa Kamati ya shule ya msingi, Mohamed Mangole, alisema kamati yake ilishauri kufungwa kwa madarasa matano na ofisi ya mwalimu Mkuu kutokana na uchakavu na kuwa ni hatari kwa wanafunzi na walimu.
“Tuliona kwa kipindi ambacho tunasubiri utatuzi wa suala hilo, mwalimu atumie jengo la choo cha wavulana ambacho hakijaanza kutumika kama ofisi kuliko kupeleka nyaraka za serikali nyumbani kwake,” alisema. Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Elias Kapama, alisema mfadhili aliyejenga choo hicho amemwambia kuwa siku za hivi karibuni atakabidhi kwa serikali ya kijiji na hivyo hajui kwa sasa atahamishia wapi ofisi yake.
Alisema matumizi ya choo hicho kama ofisi yamemwathiri kisaikolojia lakini ameendelea kukabiliana na mazingira hayo kwa kufanyakazi bila kukata tamaa na kuhakikisha kiwango cha taaluma hakishuki.
Katika shule ya Msingi Bwilingu B, kuna msongamano mkubwa wa wanafunzi madarasani kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa kwa kuwa kuna vyumba vitano huku kimojawapo kikitumika kama ofisi.
Baadhi ya walimu wakizungumza na NIPASHE kwa sharti la kutotajwa majina yao, walisema ni kawaida kwa shule hiyo darasa moja kuwa na wanafunzi 200 kwa wakati mmoja hali inayomwia vigumu mwalimu kufundisha inavyotakiwa.
Alisema pia wanafunzi na walimu wanaambukizana magonjwa ya ngozi kama mapunye na kwamba yanapoanza hujikuta hata mwalimu yanamshambulia kutokana na msongamono.
“Kama unavyoona msongamaono ni mkubwa, wanafunzi wanakaa chini na wachache kwenye madawati, walimu hatuna samani tunatumia madawati ya wanafunzi kama meza, tunaumia mgongo,” alisema mmoja wa walimu.
Shule ya msingi Kibiki, walimu wa kike na wa kiume wanalazimika kutumia choo kimoja kutokana na uhaba wa vyoo huku wanafunzi 312 wa kike na kiume wakitumia matundu mawili.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Joshua Kipoti, alisema shule hiyo ina vyumba vinne vyenye madawati 10 kila darasa na wanafunzi husoma wakiwa wamekaa chini.
Mathalalani, alisema kati ya wanafunzi 312 waliopo, wanafunzi 192 wanakaa kwenye madawati na wanafunzi 120 wanakaa chini.
Alisema shule hiyo ina walimu wanane na mwalimu mmoja analazimika kufundisha vipindi 32 kwa siku huku kukiwa hakuna nyumba za walimu.
Diwani wa kata ya Bwilingu, Ahmed Nassar, alisema kwa ujumla changamoto za elimu katika kata hiyo ni nyingi kutokana na shule za msingi kuwa katika hali mbaya.Alisema tatizo la shule za kijiji hicho amezifikisha Halmashauri na imekuwa na ahadi za kuzishughulikia.
Alisema kata hiyo ina vijiji saba vya Msolwa, Mdaula, Chahua na Matuli vyenye serikali ya kijiji na vijiji viwili vya Majengo Mapya na Mtambani havina uongozi kwa kuwa ni vipya. Mbunge wa jimbo la Chalinze, Said Mbwanamdogo, alisema shule za jimbo hilo zinamapungufu mengi ikiwamo uhaba wa madarasa, ofisi na nyumba za walimu, madawati na vyoo.
Alisema anasubiri fedha za Mfuko wa Jimbo ambazo zitaelekezwa katika ujenzi wa madarasa na ununuzi wa madawati.
Alisema mwamko wa jamii kushiriki kwenye masuala ya maendeleo ya elimu ni mdogo na walishindwa kuchangisha fedha kutoka kwa wazazi kutokana na hali ya njaa iliyokuwepo na kwamba baada ya mavuno wanaweza kuchangisha.
Ofisa elimu ya msingi wa Wilaya ya Bagamoyo, Abdul Buheki, alisema wilaya inatambua matatizo yaliyopo kwenye shule hizo na leo wanatarajia kufanya kikao na kamati ya shule na uongozi wa kijiji kutatua matatizo hayo.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment