Friday, 6 September 2013

Kikwete na Kagame "NO MORE VIJEMBE" wamaliza tofauti zao

RAIS Jakaya Kikwete amekutana kwa faragha na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, katika mazungumzo yaliyokwenda vizuri na kuwaridhisha viongozi hao wawili wa nchi jirani.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya kuibuka msuguano wa maneno ya kejeli na vitisho kwa pande zote mbili kufuatia Rwanda kupinga ushauri wa Rais Kikwete wa kuitaka serikali yake akae na waasi ili kumaliza mapigano yanayoendelea.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari, viongozi hao walikutana jana kwa zaidi ya saa moja katika mkutano uliofanyika kwenye Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, nje kidogo ya mji wa Kampala, nchini Uganda.

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete na Rais Kagame walikubaliana kuendelea kushirikiana katika kujenga uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Viongozi hao wawili wako nchini Uganda kuhudhuria mkutano wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Kimataifa wa Maziwa Makuu unaofanyika nchini humo.
Viongozi wengine ambao wanahudhuria mkutano huo ni pamoja na Rais Yoweri Museveni wa Uganda (mwenyekiti wa umoja huo na mwenyeji wa mkutano huo), Rais Silva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).
Rais Kikwete na ujumbe wake waliwasili Kampala jana asubuhi akitokea mjini Dodoma ambako aliwasili juzi jioni kwa ajili ya hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu watatu na naibu makatibu wakuuu wawili iliyofanyika Ikulu ndogo, Dodoma.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alilieleza Bunge kuwa Tanzania haina mgogoro wowote na Rwanda lakini katika kuondosha tofauti zilizojitokeza, Rais Kikwete alimwomba Rais Museveni wa Uganda awakutanishe na Rais Kagame.
Pinda alikuwa akijibu swali la kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani, Freeman Mbowe, ambaye alitaka kujua msimamo wa serikali ni kwa nini isiunde chombo cha wataalamu wa ndani ya nchi ili kushughulikia mgogoro huo.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment