Akizungumzia tukio hilo kwenye Hospitali ya Aga Khan Nairobi, mke wa mlinzi huyo, Eunice Kavesa alisema ameuona mwili wa mumewe na kusema una matundu manane ya risasi alizopigwa na magaidi hao.
Alisema aliuawa baada ya walinzi wenzake kumwita getini ili kuzungumza na magaidi hao ambao walikuwa wamekataa kupekuliwa.
“Walikataa kukaguliwa ndipo walipomwita mume wangu ambaye ni mkuu wa ulinzi hapo na alipofika tu wakammiminia risasi nane hapohapo,” alisema mama huyo.
Alisema mume wake alihamishiwa katika kituo hicho akitokea Mombasa wiki moja iliyopita na siku mauti yalipomkuta ilikuwa ni siku yake ya nne tangu alipoanza kazi hapo.
“Ameniachia watoto wawili niliozaa naye na yuko mwingine, maisha yatakuwa magumu kwa kuwa ninafanya kazi za kawaida tu na yeye ndiye aliyekuwa akitunza familia,” alisema Eunice.
Wakati akisema hayo mashambulizi yalikuwa yakiendelea katika eneo hilo la Westgate ambalo limezingirwa na vikosi mbalimbali vya usalama vya ndani na nje ya Kenya. Jana ilikuwa siku ya tatu tangu magaidi hao walipoliteka jengo hilo na kuua watu 62 huku wakiwajeruhi 175
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment