Waliosema ‘kabla hujafa hujaumbika’ hawajakosea…ni msemo wenye maana kwamba kabla ya mtu kufa, hali aliyozaliwa nayo inaweza kubadilika kuwa mbaya au nzuri au kubaki kama ilivyo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita nilikuwepo mkoani Tanga baada ya kualikwa na taasisi moja kuwa mmoja wa wazungumzaji kwenye semina ya vijana.
Nikiwa huko niliyaona na kuyasikia mengi, mojawapo ni kuhusu Akida Athuman (pichani), aliyeishia kulipwa fidia Sh108,000 tu baada ya kupofuka macho akiwa kazini wakati huo akifanya kazi katika Mamlaka ya Bandari Tanga.
Kwa bahati mbaya kwa sasa Akida haoni kabisa japo ukimwangalia unaweza kufikiri anaona, hiyo inamsababishia kushindwa kupita hapa na pale kuisaka ile anayodai haki yake inayopotea.
Anasema kuna wakati aliwahi kwenda maeneo mbalimbali yakiwemo Chuo Kikuu cha Dar esSalaam kuonana na wanasheria wamsaidie, lakini aliishia njiani kutokana na kukosa nauli.
“Ni jambo linaloniumiza, naamini iko siku Mungu atajibu maombi ya kupewa haki yangu stahiki, inaumiza sana kila ninapofikiria kwamba leo mimi sioni, tena nimeumia kazini, nimeishia kulipwa fidia ya Sh108,000 tu, sina msaada wowote kwa sasa,” anasema
Akida Athuman, ambaye anadai aliwahi kufanya kazi katika Mamlaka ya Bandari Tanga, aliumia akiwa kazini, akaishia kulipwa kile anachodai ni fidia finyu.
Historia ya Akida
Anasema alizaliwa Jijini Tanga mwaka 1951, hakumbuki tarehe wala mwezi. Ni mtoto wa nne kati watano wafamilia ya baba Addy Athuman na mama Deuli Akida.
Elimu ya msingi aliipata katika Shule ya Msingi Makolola, mkoani Tanga, alimaliza mwaka 1968. Hakuweza kuendelea kutokana na uwezo duni wa kifedha wa wazazi wake, hivyo akajiingiza katika shughuli za hapa na pale za kusaka kipato.
Mwaka 1969 alikwenda Ruvuma kusaka maisha, baadaye alipata fursa ya kuajiriwa na RTC (RegionalTrading Corporation) yaani Kampuni ya Biashara ya Mkoa.
Anasema mojawapo ya vipaji alivyonavyo ni kucheza mpira hasa safu za ulinzi, ndipo Mamlaka ya Bandari Tanga, ikamchukua mwaka 1975.
Mkasa ulivyomtokea
Mwaka 1987 ndipo mkasa huo wa kupofuka macho ulipompata.Anasema siku moja akiwa kazini, ghafla ulitokea upepo mkali, ambao ulipeperusha kemikali na saruji iliyomwingia machoni.
“Inavyoonekana ni kwamba saruji na hiyo kemikali ilikuwa imepasuka, hivyo upepo mkali ulipokuja, kemikali na ile saruji iliingia machoni…sikuona kama ni tatizo…nikaenda nyumbani kama kawaida, cha kushangaza ni kwamba nilipoamka asubuhi macho yalikuwa yanauma sana,” anasema.
“Nilifikiri ni tatizo dogo, kumbe ndiyo hivyo limebadili maisha yangu, kwamba sasa siwezi kabisa kuona.
“Macho yaliendelea kuuma, nikalazimika kwenda hospitali mbalimbali kusaka tiba bila mafanikio. Miezi mitatu baadaye nikaona niende Hospitali ya Bombo, ambako waliniangalia wakasema zile kemikali zimeharibu macho yana vidonda.
“Nikalazimika kwenda KCMC, lakini ilionekana kwamba hakuna namna ya kufanya. Mwaka 1990 ndugu zangu walinipeleka Nairobi kwa ajili ya matibabu zaidi, hali iliendelea kuwa mbaya kwamba nina vidonda na sitaweza kuona. Kuna baadhi ya vitu vilibadilishwa kwenye macho, sikuweza kuwa na uwezo wa kuona.
“Mwaka 1994 baada ya kubainika kwamba sitaweza kupona, nilishawishiwa kuacha kazi kwa maelezo kuwa mamlaka ilikuwa na mpango wa kupunguza wafanyakazi, kwa hiyo ni vizuri niombe kuacha kazi mwenyewe kabla ya kuondolewa, nilifanya hivyo.
“Mwaka huohuo, nikalipwa mafao yangu ya Sh108,000. Hali ya maisha ni ngumu mno, sina akiba yoyote ya kuniwezesha kuendesha maisha. Wakati huo naondoka kazini nilikuwa nina watoto nane,” anasema na kuongeza kuwa kwa sasa ana jumla ya watoto 11.
Anasema anashindwa kufanya chochote kupata kile anachosema haki yake iliyopotea kwa sababu hana uwezo wa kuona.
“Mtu akiniangalia anaweza kufikiri naona, kumbe sio, sioni kabisa, hata hivyo kwa sababu ni mwenyeji wa Tanga, nimezaliwa na kukulia hapa, huwa naweza mwenyewe kutembea, napanda daladala kwenda ninakotaka na kurudi kwangu,” anasema Akida, huku akiiomba Serikali na Rais Jakaya Kikwete kumsaidia kwani anasema haoni kama ni sahihi kulipwa kiasi hicho kwa ulemavu aliopata.
Kati ya watu ambao anawashukuru ni mkewe, Fatuma Juma kwani hata baada ya kupata ulemavu ameendelea kuonyesha kumpenda na kushirikiana vizuri.
“Baada ya kupata ulemavu, tunaendelea kuishi vizuri, watoto watatu wamezaliwa nikiwa sioni, nijambo linalonipa faraja, kwani wapo ambao wanapokuwa na matatizo au mmoja kuwa na ugonjwa hukimbiana,” anasema Akida
chanzo:daima
Hiyo ndio fidia ambayo serikali yetu imeona inafaa, inaangalia na kubadilisha mengine lakini sio hili. ninakofanyia kazi mimi mfanyakazi alikatika kiganja chote alichoambulia ni hiyo 108000 na kuachishwa kazi juu kwamba ni disable asingeweza kufanya kazi tena. wako wapi wanaopigania haki za wafanyakazi?? wako wapi wanaopigania haki za wanachi wa kawaida?? hivi hawalioni hili au wamejirestisha in peace tu?? nahisi naanza kupata hasira naomba niishie hapa
ReplyDelete