BOSI wa NSSF aliyeuawa kikatili kwa kuchinjwa eneo la Moshono jijini Arusha, Regina Mushi amezikwa rasmi kijijini kwao Karansi, Kitongoji cha Ashengai, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro Jumamosi wiki iliyopita.
Akizungumza wakati wa mazishi hayo baba mzazi wa marehemu, Damas Mushi alilaani tukio la kuuawa kikatili kwa binti yake huyo ambaye miaka michache iliyopita alihitimu shahada yake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuajiriwa katika Taasisi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambapo alifanya kazi miaka miwili hadi kifo kilipomkumba Oktoba 14, mwaka huu nyumbani alipokuwa akiishi Moshono, jijini Arusha.
Regina aliuawa kinyama chumbani kwake kwa kuchinjwa na kukatwakatwa sehemu mbalimbali za mwili wake na hadi sasa haijafahamika sababu ya kufanyiwa unyama huo.
“Siku chache kabla ya kifo cha mwanangu aliniambia kuwa ana mpango wa kuendelea kusoma kwa kiwango cha shahada ya pili lakini bahati mbaya ameuawa kikatili ni jambo la kusikitisha sana,” alisema mzazi huyo.
Ametoa wito kwa jeshi la polisi kuhakikisha linafanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo ili kuwabaini na kuwatia mbaroni waliofanya unyama huo.
Naye baba mdogo wa marehemu, Wakili Cornelius Kariwa amesema mauaji hayo ni kinyume cha sheria na ni kitendo cha kishetani.
Naye baba mdogo wa marehemu, Wakili Cornelius Kariwa amesema mauaji hayo ni kinyume cha sheria na ni kitendo cha kishetani.
“Ukatili wa namna hiyo wa kumchoma mtu visu ni wa hali ya juu kwani ulisababisha kutapakaa na kujaa damu kitandani, ni ukatili uliopitiliza ambapo hata angekuwa na kosa marehemu asingepaswa kupata adhabu ya aina hiyo na kwamba kitendo hicho ni cha kulaaniwa katika jamii,” alisema wakili huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Liberatus Sabas amethibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo,” alisema kamanda huyo.
chanzo:globalpublishers
No comments:
Post a Comment