MKAZI wa Nyamakokoto mjini Bunda, Mara, Athuman Peter, maarufu kama Mzee wa Genya (26), amehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Bunda kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumnyang’anya sh 100,000 na simu ya kiganjani mama yake mzazi kwa kutumia silaha.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Bunda, Saidi Kasonso, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Masoud Mohamed, kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Novemba 18, mwaka jana, saa 1:30 jioni, katika Mtaa wa Nyamakokoto, mjini Bunda.
Mohamed alisema kuwa siku ya tukio mshtakiwa huyo alimvamia mama yake mzazi, Pendo Mgasa, aliyekuwa nyumbani kwake na kumnyang’anya fedha hizo taslimu pamoja na simu ya mkononi aina ya Nokia yenye thamani ya sh 20,000.
Alisema kuwa katika kufanya unyang’anyi huo, mshtakiwa huyo alitumia panga alilokuwa nalo, akimtishia kumuua mama yake endapo angekatalia fedha hizo au kufanya lolote.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Kasonso alisema kuwa ameridhika pasipo kuacha shaka yoyote juu ya ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na kwamba kwa jinsi hiyo anamtia hatiani mshtakiwa huyo kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela.
Alisema kuwa kitendo alichokifanya mshtakiwa huyo ni cha kinyama hasa kwa mama yake mzazi na kuongeza kuwa adhabu hiyo itakuwa fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo ya kutaka kujipatia fedha na mali kwa njia za unyang’anyi.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alipotakiwa kujitetea alishindwa kufanya hivyo na badala yake alibaki kimya bila kusema lolote.
Chanzo:daima
No comments:
Post a Comment