WANANCHI wa Kijiji cha Minziro, Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, wameyakimbia makazi yao baada ya kundi kubwa la askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuvamia na kuwashambulia raia kisha kuchoma moto nyumba zao.
Wanajeshi hao wakishirikiana na askari polisi, Usalama wa Taifa na maofisa wengine wa serikali, wapo mkoani Kagera wakiendesha Operesheni Tokomeza Ujangili inayoendeshwa nchini nzima katika hifadhi za taifa kwa lengo la kukabiliana na ujangili wa kuua tembo pamoja na uvunaji haramu wa mazao ya misitu.
Katika tukio hilo lililotokea Oktoba 13 mwaka huu, baadhi ya waumini waliokuwa wakitoka katika Kanisa Katoliki Parokia ya Minziro, walijikuta wakikumbana na kipigo ambacho baadhi yao kimewaacha na majeraha makubwa.
Wanajeshi hao wanadaiwa kuwafunga kamba wananchi na kuwaning’iniza kwenye magari yao, huku wakiwapa mateso makali.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mulungu ‘A’, Boniface Ponsian, alisema kuwa wananchi wengi wameyahama makazi yao kutokana na hofu ya kuumizwa na askari hao ambao waliendesha kipigo kwa siku mbili mfululizo.
Alisema askari hao ambao hawakuwa na hata chembe ya huruma, walikuwa wakiendesha vipigo kwa kila mtu aliyepita mbele yao, tukio lililowagusa hata wapita njia kutoka maeneo mengine nje ya kijiji hicho.
Ponsian alisema katika tukio hilo, zaidi ya wananchi 20 wa Kijiji cha Minziro waliumizwa vibaya na askari hao ambao wanadaiwa kuwapa mateso ya kila aina wakiwahusisha na wahamiaji haramu kutoka nchi za Burundi, Rwanda na Uganda.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, wanajeshi hao baada ya kutembeza kipigo kwa siku mbili mfululizo, walichoma moto nyumba za wananchi yakiwamo maduka na kubomoa baadhi ya milango ya nyumba hizo.
Aliwataja baadhi ya waathirika walioshambuliwa na askari hao kuwa ni Josephat Joseph, Edwin George, Didas Domisheni, Steven Serapioni, Sonko Yoronimu, Mukasa Mathias na Josephat Emmanuel.
Alisema kuwa askari hao pia walilichoma moto duka la mfanyabiashara Joseph Jovin wa Kijiji cha Minziro ambaye amekimbia makazi yake sanjari na Edward Mgowa ambaye wanajeshi hao walibomoa milango ya nyumba yake na hivyo kulazimika kukimbilia kusikojulikana pamoja na mkewe huku wakiwaacha watoto wao watano.
Katika tukio hilo, askari hao walimuumiza vibaya Josephat Emmanuel baada ya kupewa adhabu ya kutembelea magoti kwa umbali mrefu huku pia akipewa kipigo kikali.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Kanali mstaafu Issa Njiku alisema hana taarifa za wananchi hao kushambuliwa na wanajeshi.
Akizumgumza na Tanzania Daima kwa simu, Njiku alisema yupo likizo, hivyo hafahamu chochote juu ya tukio hilo, licha ya ukweli kwamba baada ya kutokea wananchi walimpigia simu na kumjulisha unyama waliokuwa wametendewa na askari hao.
Utetezi wa mkuu wa wilaya, ulifanana na ule wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Phillip Kalangi, ambaye naye alidai hajapata taarifa kutoka kwa OCD wa Wilaya ya Misenyi juu ya tukio hilo, hivyo akaomba apewe muda ili afuatilie.
Kamanda Kalangi alisema amefanya mawasiliano na OCD wake wa Misenyi bila mafanikio, kwamba alikuwa nje ya mtandao wa mawasiliano kutokana na kuwa eneo lisilokuwa na mawasiliano
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment