NAONA Mpemba leo kaingia na tasbihi mkononi akijikumbusha enzi zake za ucha Mungu. Kila mtu anamshangaa akiwa na mshawasha wa kujua kulikoni.
Anaamkua: “Assalaam Alaykum Jamia.” Wote tunajibu: “Walaykum Salaam Warrahmatullahi wabaraakaatuhu.”
Mgosi Machungi anamchokoza. “Sheikh leo kunani mbona umeingia kinamna na zana za masharifu? Hebu tiambie umeota nini hadi unaingia na zana hizi za maangamizi ya mafirauni?”
Mpemba anajibu: “Nimeamua kumshukuru Subhanna kwa kumnusuru ndugu yangu alokwenda hijja Makka na kurejea bila kukamatwa na bwimbwi yakhe.”
Mgosi anajibu: “Ni jambo la kumshukuu Mungu. Maana Wabongo siku hizi kila wanapokwenda wanashukiwa kuwa makontena.”
Kabla ya Mgosi kuendelea, Mijjinga anakatua mic. “Tena umenikumbusha. Mmesikia rais alivyosema kuwa sasa tutaje wauza bwimbwi? Inaonyesha ameamua kuwashughulikia.”
Msomi Mkatatamaa anatia buti. “Bado kuna watu mnaamini hizi sanaa na ngonjera usawa huu?”
Mgosi anauliza: “Una maana hizi ni sanaa kama kawa Msomi?”
Msomi anajibu: “Mimi nawafahamu wengi. Hata rais mweyewe anawafahamu vizuri sema hajawa na nia ya kweli ya kuwashughulikia kwa sababu ajuazo mwenyewe.”
Anaendelea: “Nawaona kila siku. Vitu vyao naviona kila siku. Lakini sitataja. Siko tayari kujidanganya na kuwadanganya wachovu. Huu kwangu ni unafiki unaonuka na wa kutisha so to speak.”
Mijjinga naye anaongezea msumari wa moto. “Kama yeye mwenye madaraka na walinzi wenye mitutu ameshindwa kwa miaka saba, sisi tutaje kama nani? Anadhani tumesahau yaliyomfika Aminia Chifwupa aliyeonyesha dalili za kutaja akakolimbiwa hata kabla ya kutaja? Go tell to the bird Mr Prezo. Haingii huu mkenge mtu.”
“Kwa vile dingi huwa anasoma minutes za vikao vyetu lazima nimpe salamu zake kupitia mkutano huu wa Kijiwe. Kwanza, yeye ataje. Maana alisema mwaka 2006 kuwa ana orodha ya wahalifu hawa. Pili, atuhakikishie usalama wetu. Tatu, ahakikishe watakaotajwa hata kama ni ndugu wanasulubiwa kama vibaka,” anazoza Kapende.
Mipawa naye anaamua kuongeza yake. “Pia lazima atoe mshiko wa kuhamia mabonde poromoka kujificha au atoe viza watu waishie zao majuu wakatanue baada ya kulipua mibomu.”
“Hivi hawa wanaotudanganya kuwa sisi tutaje kwa vile wao hawajui wanaishi wapi? Mbona kila mchovu na mzito anawajua hawa jamaa! Pale Kinondoni wanapima kwa ukucha tena kwa soo tatu tu,” anachomekea Mbwa Mwitu huku akitupa kipisi chake cha sigara kali.
Msomi anarejea na kusema: “Tuambizane ukweli. Kinachoendelea ni usaliti kwa kaya. Hivi hawa wanaojifanya hawajui wauza bwimbwi wanatuona sisi hamnazo siyo? Mbona wamejaa mateja mitaani? Ukiamua kula nao sahani moja unawapata wanaowauzia huo unga. Tukubaliane kuwa hatutaki kuwashughulikia hawa wahalifu kwa vile tuna maslahi yetu kwenye jinai hii. Sioni hata sababu ya kupotezeana muda kujadili vitu visivyowezekana. Kwani nani mwenye mamlaka kisheria kuwashughulikia? Kama wenye madaraka wanayakalia na kuwalea hawa wahalifu mnadhani sisi wachovu tutaweza?”
“Mwenzenu sitaji majina. Ngoja nimtajie dingi makao makuu ya mtandao huu. Kama anataka kufanya kweli basi aanzie pale Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Mchonga wanakopitisha mchana kutwa,” anasema Mchunguliaji.
Mipawa naye hataki kuachwa nyuma. Anakwanyua mic: “Kweli hawa wanaosemaga tutajage wanatuona wajinga. Hata nao wanawajua hawa washenzi. Mbona mijibaba inayofugaga ukucha mmoja mkubwa sana wanaifanyiaga kazi gani kama siyo kipimio ni nini? Ikamatege uisweke ndani utajua mengi.”
“Usemayo ni kweli mtani. Wanakijiwe tunajua mengi. Tunakunywa kahawa nao, kwenye mbavu za mbwa tuko nao, maghorofani hata ma BMW tuko nao. Jitu linalala apache alolo linaamka tajiri na hakuna anayehoji,” anachomekea mzee Maneno huku akipokea kipisi toka kwa Kapende.
Leo Msomi ameamua kutawala kijiwe. Kwani anaamua kuchangia tena. “Rudisheni maadili ya Mchonga muondoe maadili ya Ruxa na ujambazi wa Nkapu. Naona heri waruhusu mibwimbwi iuzwe kama sigara kama alivyosema munene ‘raha jipe mwenyewe. Kizuri shurti na mwenzio.’ Hii iitwe kaya ya Bwimbwi ambapo kila mtu akifanya biashara hii atakuwa tajiri na tutaachana na kumtesa mnene kwenda kombe mkononi akibomu ughaibuni kila siku.”
Anakunywa kahawa yake na kuendelea: “Mibwimbwi ikiruhusiwa hata hao wauza wataonja na kununua kwa wengine. Tuchague kukamata wauza au kuruhusu bwimbwi liwe bidhaa halali kama fegi. Mie naona waruhusu tu maana if you can’t beat them just join them and enjoy with them whatever they’ve.”
Bi Sofi Kanunga ambaye alikuwa kimya kwa muda mrefu anaamua kukatua mic. “Mie naona tusiwe na haraka. Kwa vile mtukufu rais amesema tutaje majina na awashughulikie, tumuamini na kuwataja wauza bwimbwi.”
Mijjinga hamkawizi. Anauliza. “Sofi vidani vyako vina harufu ya mibwimbwi. Unapiga umbea kwa sana, lakini unapanga midhahabu pesa yatoka wapi?”
“Kaka Mijjinga naona unaanza kunichimba. Sitaki utani huu mbaya wa kunihusisha na balaa la bwimbwi nasema.”
“Anakuchimba wapi na kwanini akuchimbe? Hebu tiambie tielewe,” anachomekea Mgosi Machungi.
Kanji ambaye ndiyo amerejea toka zake Bombay anaamua kukatua mic kwa mara ya kwanza. “Chungi tani nyingine baya sana. Mimi jua sana Bi Sofi, hapana uza bimbi iko safi kabisa.”
Mgosi hakubali. Anajibu: “We Kanji unamjua vipi Bi Sofi. Hebu tieleze vizui tijue. Kwani hizi gold za Sofi zina alama? Titajuaje kama ni matokeo ya pesa ya bwimbwi? Au nawe ni wale wale? Nitakutaja mie angalia sana. Kila maa unakwenda Bombay. Hiyo njuuku unaipata wapi kama hakuna namna?”
“Chungi iko heshimu veve. Mimi uza unga ya kula si unga ya kubia bwana,” anajitetea Kanji.
Msomi kuona utani unaanza kuharibu mada aliingilia tena. “Tuwe wakweli. Kama mkuu ameshindwa kutaja, anadhani sisi tumeumbwa kwa mawe tufanye hivyo halafu awe shahidi wa kuona tukikolimbwa kama Aminia Chifwupa siyo? Naona wanakamata kwa midomo huku wakiwanyotoa roho wale wanaowafichua hawa wadudu.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinaanza kunoga si mshangingi wa bei mbaya wa zungu la unga ukapita. Tulianza kuzomea kwa sana tu. Baada ya kuona zungu la unga linabonyeza simu yake kila mmoja alijikata kivyake ili ndata wasije wakatubambikia kesi kulinda zungu lao linalowapa mshiko.
Tulitawanyika tukiimba: “Mkuu taja kwanza ndipo nasi tutaje vinginevyo ni kamba.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment