Thursday, 24 October 2013

Mbunge CCM aolewa na kinda,ana miaka 60 kijana 26.

MBUNGE wa Viti Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rosweeter Kasikila (60), amejikuta kwenye kashfa nzito ya kufunga ndoa na kijana, kinda wa miaka 26, Michael Christian.
Ndoa hiyo ambayo ilifungwa katika Kanisa la Tanzania Assembles of God (TAG), linaloongozwa na Mchungaji Getrude Rwakatare ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM, imebaki kuwa gumzo na kuwaacha hoi baadhi ya mawaziri, wabunge wanaoifahamu pamoja na majirani wanaoishi na mbunge huyo.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya wanandoa hao na majirani wanaowazunguka, vililiambia gazeti hili kuwa ndoa hiyo ilifungwa Septemba Mosi mwaka 2011, na imebaki kuwa siri kabla ya wawili hao kukorogana.
Kabla ya wawili hao kuamua kufunga ndoa, mbunge huyo kutoka mkoani Rukwa, mwenye makazi yake Bagamoyo mkoani Pwani, alikuwa akimtumia Michael kwenye shughuli mbalimbali na muda wote alikuwa akiishi nyumbani kwa mbunge huyo.
Inaelezwa kuwa mbunge huyo ambaye ana familia ya watoto wawili ambao kiumri wanalingana na Michael, alianza uhusiano wa kimapenzi na kijana huyo kwa siri kubwa na baadaye alifanikiwa kumshawishi wafunge ndoa huku akimuahidi kumpa huduma mbalimbali anazotaka.
Kwa mujibu wa habari hizo, wawili hao waliamua kufunga ndoa katika Kanisa la TAG baada ya mbunge huyo kufanikiwa kumshawishi Mchungaji Rwakatare kwamba ndoa hiyo itakuwa siri, hasa kutokana na tofauti ya kiumri kati yao.
Hata hivyo ndoa hiyo kwa sasa imekumbwa na mgogoro mkubwa, huku mbunge huyo akidaiwa kuzuia kila kitu cha mumewe huyo, hasa vyeti vyake vya shule kama njia ya kumbana warudiane.
Siku ya harusi
Kwa mujibu wa mashuhuda wa harusi hiyo ya aina yake, mbunge na kijana huyo walikwenda kanisani wakiwa wawili bila mashahidi kama ilivyo kawaida, na ndoa hiyo ilifungwa katika ofisi ya kanisa na sio ndani ya kanisa.
Mashahidi wa ndoa hiyo waliitwa hapo hapo kanisani na walisimamia na kushuhudia utiaji saini wa cheti cha ndoa na kisha wanandoa hao kutawanyika kwenda kwenye fungate (Honey Moon). Hakukuwa na sherehe baada ya kufungwa ndoa.
Inadaiwa kuwa hakukuwa na ndugu yeyote wa maharusi hao aliyeshuhudia tukio hilo la kihistoria la wawili hao kuunganishwa na kuwa mwili mmoja.
Kauli ya Bwana harusi
Tanzania Daima Jumatano, lilifanikiwa kumpata Michael, ambaye katika mazungumzo yake alikiri kufunga ndoa na mbunge huyo Septemba Mosi mwaka 2011, lakini kwa sasa wametengana kutokana na sababu ambazo hakutaka kuziweka wazi.
“Mimi nadhani hili ni jambo binafsi, sio vizuri kulizungumza hadharani ila kweli nilifunga naye ndoa maana inaonekana mnajua mambo mengi kunihusu, na ni kweli kwa sasa tumeachana,” alisema kwa kifupi.
Alisema walikutana na mbunge huyo Bagamoyo wakati alipokuwa akifanya mafunzo kwa vitendo katika hospitali ya wilaya hiyo kama muuguzi mkunga wakati mbunge huyo akiwa muuguzi mkuu wa wilaya katika hospitali hiyo.
Alipoulizwa sababu za kukubali kufunga ndoa na mama wa umri wa miaka 60 wakati ana miaka 26 na sababu za ndoa hiyo kuvunjika, Michael alisema ana historia ndefu katika maisha yake kwani alizaliwa yatima na amekua na kulelewa kwa ufadhili wa kituo  cha Safina Street Network.
“Katika mazingira niliyokulia, unaweza kujua kwanini nilikubali kuingia kwenye ndoa hiyo. Sina ndugu hata wa kunishauri. Hata hivyo, hayo tuyaache. Lakini ukweli ndio huo, lakini kwa sasa tumeachana, kila mtu ana maisha yake,” alisema Michael kwa masikitiko.
Michael ambaye kwa sasa anasoma katika Chuo Kikuu cha Muhimbili, pia alikiri kuwa mbunge huyo anashikilia vyeti vyote vya shule ambavyo anavihitaji sana kwa ajili ya kusaka ajira baada ya kumaliza masomo yake Muhimbili.
Alitaja sababu ya kuvunja ndoa hiyo kuwa ni manyanyaso kwa vile ni mdogo na masikini kwani hakuwa na sauti na alibanwa kwa kila kitu kiasi cha kukosa kabisa amani katika maisha yake.
“Kimsingi ndoa yangu na mama imevunjika na ilivunjikia mikononi mwa Rwakatare wakati akijaribu kutusuluhisha, alinitaka nirudi kwa mama, hapana, siko tayari na hapa nataka vyeti vyangu tu basi,” alisema Michael.
Mbunge ang’aka
Kwa upande wake, mbunge huyo alipoulizwa, kwanza alikuwa mbogo na kukataa katakata kuzungumza kwa madai kuwa hawezi kuzungumzia jambo hilo zito kwenye simu.
Mbunge huyo alikiri kuwapo kwa ndoa hiyo, lakini alipinga kwamba haijavunjika na kumhoji mwandishi wa habari hizi kama anajua taratibu za kuvunja ndoa.
“Michael kakuambia hiyo ndoa imevunjika? Wewe si unajua taratibu za ndoa kuvunjika? Kwanza nimeshasema sitaki kuzungumzia suala hili kwenye simu ukitaka tuonane kesho kwani kuna haraka gani? Jambo la haraka ni la mjamzito kutaka kujifungua, lakini kama ni suala hilo hakuna sababu ya uharaka,” alisema mbunge huyo.
Hata hivyo baada ya kubanwa, mbunge huyo alimtaka mwandishi wa habari hizo kukutana naye katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata ufafanuzi, lakini cha ajabu mwandishi alipofika katika ofisi hizo hizo, mama huyo alizima simu yake na  hakupatikana tena.
Mchungaji Rwakatare
Alipotakiwa kuzungumzia ndoa hiyo, Mchungaji Rwakatare kwanza aling’aka kwamba hajawahi kufungisha ndoa ya aina hiyo.
Lakini alipobanwa alikiri kuikumbuka ndoa hiyo na kwamba ilifungishwa na mchungaji wa kanisa lake, aliyemtaja kwa jina la  Mchungaji Mtetumo.
Alimtetea mchungaji wake kwamba alichokifanya ni kutimiza wajibu wake wa kichungaji wa kufungisha ndoa, hasa kama wanandoa wametimiza vigezo.
“Wajibu wa kanisa ni kufungisha ndoa, kama wanandoa wamekidhi vigezo vya kanisa. Sio kazi ya kanisa kuwachagulia wachumba kwa maana hakukuwa na sababu ya kuhoji umri wao, wala jambo lolote zaidi ya kufungisha ndoa hiyo,” alisema Mchungaji Rwakatare
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment