Tuesday, 22 October 2013

Nyama ya ng’ombe yawagonganisha CCM

DIWANI wa Kata ya Kinyeto, Francisco Ng’eni (CCM), ametuhumiwa kuiba nyama ya ng’ombe iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya sherehe za kufunga kambi ya vijana wa UVCCM katani humo, Wilaya ya Singida.
Habari za uhakika zinadai kuwa vijana hao walikuwa wameahidiwa kupewa ng’ombe mmoja kwa ushawishi wa Justine Monko ambaye inasemekana ameanza kujipanga kuwania ubunge wa Singida Kaskazini.
Lakini diwani huyo anadaiwa kuchakachua nyama hiyo na kutoa kilo kumi badala ya mia moja.
Kwa mujibu wa habari hizo ambazo zimethibitishwa na mmoja wa viongozi wa UVCCM wa Kata ya Kinyeto, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake akihofia nafasi yake ya uongozi, baada ya vijana kuona kiasi hicho cha nyama waligoma isipikwe kwa madai kuwa hakuwa ng’ombe mzima.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa diwani huyo alilazimika kufanya kazi ya ziada kuwaomba vijana hao wakubali kuchemsha kiasi hicho cha nyama iliyokuwepo ili kumfichia kashfa hiyo asionekane amewasaliti kwa kutokutimiza ahadi ya mjumbe aliyetoa ng’ombe huyo.
Taarifa kutoka Kinyeto zinasema kuwa Ng’eni alikuwa akiwashawishi vijana hao wasipokee msaada wa mchele na mafuta ya kupikia vilivyotolewa na mbunge wa jimbo hilo, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Ng’eni ambaye anadaiwa kuwa mfuasi wa Monko, alidai Nyalandu alijifanya kuwa na majukumu mengi akamtuma mkewe kupeleka misaada hiyo.
Taarifa zinadai kuwa kumekuwepo na kutokuelewana baina na Ng’eni na Nyalandu kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kutokana na harakati za baadhi ya wajumbe kuanza jalamba la kuwania ubunge jimboni humo.

Hata hivyo, baada ya mvutano wa muda mrefu ndipo ilibainika kuwa nyama iliibwa, lakini wakati huo vijana wengi walikuwa wameishaondoka wakikataa uchakachuaji huo, huku wengine wakihoji yalikopelekwa makongoro.
Alipotafutwa kujibu tuhuma hizo, diwani huyo alisema Nyalandu ana dharau, alimtuma mke wake kupeleka msaada lakini vijana waliukataa na kwamba hilo la kuiba nyama analisikia kwa mwandishi.
“Niambie wewe umeambiwa na nani ili nijue kama ni za kweli au sio kweli,” alisema.
UVCCM walikuwa wameweka kambi ya siku tano katika Kata ya Kinyeto kuanzia Oktoba 13 hadi 17 mwaka huu, ambayo ilifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga.
Kongamano hilo lilifungwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai huku kukiwa na tafrani za kutoelewana baada ya vijana kumtuhumu diwani kwa kuchakachua vyakula vilivyotolewa.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment