Tuesday, 22 October 2013

Waliokamatwa wakifanya mafunzo ya kigaidi msituni washtakiwa.





HATIMAYE watuhumiwa 11 ambao walikamatwa wakifanya mafunzo ya kigaidi kwa kutumia CD za Al Shabaab na Al Qaeda katika msitu wa Makoloanga wilayani Nanyumbu, mkoa wa Mtwara, wamefunguliwa mashtaka mawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawadhi Mkoa wa Mtwara, Dynes Lyimo, waendesha mashtaka wa serikali, Peter Musetti, na Ladislaus Komanda, jana waliieleza mahakama kuwa September 21 na 26 mwaka huu, maeneo ya msitu wa Makoloanga, washtakiwa hao kwa pamoja walifanya mkusanyiko usiokuwa halali na kusababisha hofu kwa wakazi wa maeneo hayo.
Kosa la pili la washtakiwa hao ni kukutwa na CD zenye mafunzo ya kigaidi ambapo ni kinyume cha sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hakimu Lyimo alisema dhamana iko wazi kwa washtakiwa kwa masharti ya kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wakazi wa mkoa wa Mtwara ambapo mmoja awe mtumishi wa serikali au taasisi inayotambulika na serikali na mali isiyohamishika isiyopungua sh milioni 5 pamoja na barua kutoka kwa mwajiri au ofisa mtendaji.
Hata hivyo, washtakiwa hao waliofikishwa mahakamani hapo ya saa 2:30 asubuhi wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi na kusomewa mashtaka yao saa 4: 30 asubuhi walishindwa kutimiza masharti hayo.
Watuhumiwa wote walikana mashtaka na wamerudishwa rumande hadi November 4 kesi hiyo itakapotajwa tena.
Watuhumiwa wawili zaidi waliounganishwa na wenzao 11, hawakufikishwa mahakamani jana kutokana na upelelezi wao kutokamilika.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment