Monday, 18 November 2013

Mitandao ya simu iwe makini na siri za wateja

Kila jambo kabla halijatoka hadharani hubakia kuwa siri kati ya mhusika au wahusika maalum, tumezoea kuwa na siri za habari, ambapo inawezekana kabisa kuwapo kwa siri nyingine za vitendo na baadhi ya matukio.
Zipo siri za taarifa au habari katika viwango mbalimbali, kuanzia siri za chini kabisa ambazo huonekana kutokuwa na madhara makubwa hata kama zikivuja ambazo huitwa 'zilizozuilika' (Restricted), zinafuatia aina nyingine ya siri kwa kiwango cha kati, ambazo zimewekewa kiwango cha 'Confidential'.
Zipo habari nyingine zinazowekewa hadhi ya usiri ambayo ni kubwa katika ngazi ya 'Secret', na mwisho kabisa ni siri zilizo katika kiwango cha juu zaidi na huwekwa katika ngazi ya 'Top secret'.
Viwango vyote vya nyaraka zilizo katika usiri wa aina mbalimbali kati ya hizo, ni kwamba hazitakiwi kusomwa au kuishia mikononi mwa wasiohusika, nyaraka hizo mara nyingi hazipatikani kiholela, na hata kama zikivuja, basi huingia katika mtandao wa mikono ya hao wasiohusika kwa tahadhari ya aina fulani.
Hakuna siri isiyojengewa tahadhari, siri za mmoja mmoja na hata siri za taasisi huwa katika mfumo wa hifadhi kabla hazijafanyiwa kazi iliyokusudiwa, na hakuna mfumo unaoweza kufanya kazi bila kuwa na utaratibu 'nyeti' wa utunzaji wa siri zake, hata katika utaratibu wa ajira, taarifa za mtu binafsi hubakia kuwa siri kati ya mwajiri na mwajiriwa.
Sehemu kubwa ya Watanzania sasa hivi wanatumia mawasiliano ya simu za mkononi, na kwa kiwango kikubwa simu hizo zimerahisisha sana upatikanaji wa habari pamoja na utendaji wa kazi za kila siku, ingawa kumejitokeza lawama za kuvujishwa kwa siri za taarifa za kwenye mitandao ya simu hizo kinyume cha sheria. Sheria husika ni ile ya Mawasiliano ya Kielekroniki na Posta ya mwaka 2010 inayotoa kina kwa mteja.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, (TCRA) na kampuni za simu za mikononi, zimewataka wateja watakaokumbwa na tatizo la kuvujishwa kwa taarifa za simu, kuripoti kwenye vyombo vya dola ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Ingawa imeelezwa kuwa zipo mashine za kuzuia taarifa za siri za simu za mikononi kutovuja, baadhi ya wafanyakazi wa kampuni za simu ambao si waaminifu wamekuwa wakihujumu wateja kinyume cha sheria kwa kuchezea teknolojia isivyopaswa.
Hadhari hiyo imekuja kukiwa na wimbi la matumizi mabaya ya simu za mkononi nchini, ikiwamo matumizi ya teknolojia kutoa hadharani mawasiliano ya siri za watu.
Ipo mifano ya matukio ya hivi karibuni, zipo taarifa zilizoanikwa kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, zikionyesha mawasiliano ya siri anayodaiwa kufanya na watu mbalimbali yakidaiwa kuwa ni ya kukihujumu chama chake.
Pia matumizi mengine ni kama aliyodai kufanyiwa Mbunge wa Arusha, Godless Lema, ambapo pamoja na namba za simu kadhaa kudai zinamtumia ujumbe wa matusi, pia alidai upo ujumbe wa matusi unaotumwa kwa watu na namba inayojitokeza ikionesha ni ya Mbunge huyo, suala alilodai kuwa limemchafua kisiasa na kijamii.
Matukio ya aina hiyo ameyazungumzia Meneja Uhusiano wa TCRA Innocent Mungy, kuwa kampuni za simu zinaongozwa kwa mujibu wa sheria, hivyo alisema hakuna kampuni itakayokubali kutoa taarifa za siri za mteja kutokana na ukweli kuwa ni hatari kwa upande wao.
Mungy alisema anachojua na ambacho kinaweza kuonekana na kupatikana kutoka katika kampuni hizo, tena kama tu zitaombwa na polisi ama vyombo vya usalama kufanya hivyo kwa kulinda usalama wa taifa, ni kwa kueleza kuwa siku fulani uliwasiliana na fulani saa fulani na kampuni zinaweza kuchapa taarifa hiyo na kuitoa ingawa haitaeleza undani wa kilichozungumzwa.
Siri lazima zihifadhiwe, na ndiyo maana Mungy alisema kampuni za simu zinao utaratibu wa mafundi wake kuingia ndani ya chumba cha kuhifadhi taarifa za siri, na ikiwa mtu anao uhakika wa namba fulani ya kampuni fulani imetumiwa visivyo, anapaswa kutoa taarifa polisi ili hatua ziweze kuchukuliwa kwani hilo ni kosa la uhalifu wa mtandaoni.
Kwa vile simu hizo sasa ndiyo tegemeo kubwa la mawasiliano kwa wengi, inatakiwa itolewe elimu ya kudhibiti taarifa wanazoona ni za siri kwa wateja wa mitandao yote, pia wafanyakazi wa kampuni zinazomiliki mitandao hiyo wanatakiwa wachukuliwe hatua madhubuti na kali mara wanapobainika kuvujisha siri za wateja wao.
Mitandao ya simu hizi kwa sehemu kubwa imechukua kazi ambazo awali zilikuwa zikifanywa na Shirika la Posta na Simu, matokeo yake shirika hilo limejikuta likipunguziwa majukumu kwa asilimia kubwa.
Mitandao hiyo pia inafanya kazi nyingi za kibenki, ushindani wa kuwashawishi wateja kutumia mitandao ya simu kwa kuweka, kutuma na kupokea fedha kwa mitandao ya simu umekuwa mkubwa kiasi ambacho kama wafanyakazi wao hawatakuwa makini kutunza siri za wateja wao, utajitokeza wizi mkubwa utakaoharibu biashara za kampuni za simu.
Ingawa kwa kiwango kikubwa tunanufaika sana na huduma nzuri za kampuni za simu, lazima tuweke tahadhari kwa ajili ya usalama wa taarifa tunazozituma ili zisivuje na kuwafikia wasiohusika, pamoja na uhakika wa usalama wa fedha zinazopitia katika mitandao ya simu hizo.
Naamini vipo vikundi vya kitapeli ambavyo kila kukicha vinanoa vichwa na kubuni namna ya kuwarubuni watu wengine kwenye mitandao kwa ajili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Ni wajibu wetu kutoa ushirikiano kwa polisi endapo mteja utagundua udanganyifu na kuvujishwa kwa siri zako kupitia mitandao.
chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment