Monday, 18 November 2013

Ndugu atoboa ndoto ya Dk. Mvungi

Wakati safari ya mwisho duniani kwa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Dk. Sengondo Mvungi, itahitimishwa leo, kaka yake, Mrindoko Mvungi, amegusia jinsi ndugu yake alikuwa ameuweka mwezi Novemba kama wakati wa kwenda kwao.

Akizungumza na NIPASHE jana kijijini kwao Chanjale juu, Kata ya Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga, mkoaniKilimanjaro, Mrindoko alikumbushia alivyozungumza na Dk. Mvungi juu ya safari hiyo ilishikamanishwa na ujenzi wa nyumba yake kijijini hapa.

“Nitarejea kijijini hapa mwezi Novemba kama mtanihakikishia kwamba niliowapa kazi ya kuujenga mji wangu watakuwa wamekamilisha na kutimiza ndoto yangu kijijini,” alisema Mrindoko, akimnukuu Dk. Mvungi walipokutana wote Septemba, mwaka huu, alipokwenda katika kikao cha bodi ya Shule ya Sekondari ya Mrindoko, ambayo alikuwa Mwenyekiti.

Alisema kuwa Dk. Mvungi alitoa kauli hiyo kutokana na nyumba yake kuharibiwa na mafundi wa ujenzi  marakadhaa na hivyo kumkasirisha.

Jambo hilo lilimfanya atamke maneno hayo miezi miwili iliyopita kabla ya kukutwa na mauti akiwa katika Hospitali ya Milpark, Johanesbarg nchini Afrika ya Kusini alikokwenda kupatiwa matibabu baada ya kuhamishwa kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).

Hata hivyo, ingawa ujenzi wa nyumba hiyo unaendelea na huenda itakamilika mwezi huu, safari ya Dk. Mvungi imefikia tamati na leo atazikwa kwenye makaburi ya familia hiyo yaliyopo kijijini hapo.

MWILI UTAKAVYOWASILI
Kabla ya kuuzika mwili wa Dk. Mvungi nyumbani kwao Chamakera, waombolezaji, wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa, serikali na wajumbe wa tume hiyo, wanatarajiwa kuwasili alfajiri ya leo na kupokewa katika viwanja vya Parokia ya Kisangara Juu, iliyopo chini ya Kanisa Katoliki, Jimbo la Same.

Ratiba iliyotolewa kwa waombolezaji na kaka mkubwa wa marehemu, Mrindoko Mvungi, inaeleza kuwa baada ya msafara uliobeba mwili wa Dk. Mvungi kuwasili kijijini hapo, waombolezaji kutoka sehemu mbalimbali nchini, wataanza kukusanyika saa 4:00 asubuhi katika Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Parokia ya Kisangara Juu.

Hapo ibada ya mazishi itafanyika, ikiwa ni pamoja na wakazi wa maeneo hayo kupata fursa ya kumuaga mpendwa wao kabla ya kwenda kuupumzisha mwili wake katika makaburi ya familia ya marehemu Mzee Adrian Mganyo Mvungi, aliyezikwa Chamakera.

“Mwili wa Dk. Mvungi utawasili hapa alfajiri ya kesho (leo) na ukifikishwa hapa nyumbani, mishale (majira) ya saa 4:00 asubuhi waombolezaji wataelekea kanisani na saa 5:00 kwa mujibu wa uongozi wa Parokia ya Kisangara Juu, misa ya mazishi itaanza muda huo saa 8:00 tutakapokwenda kumhifadhi katika makaburi ya familia ya Mvungi,” alisema Mrindoko.

Kwa mujibu wa Mrindoko, ibada ya mazishi itaongozwa na Askofu Rogath Kimaro wa Dayosisi ya Same ya Kanisa Katoliki, akisaidiwa na Mkuu wa Parokia hiyo, Padri Wilhad Mbombengwa.

Dk. Mvungi ni mtoto wa sita kuzaliwa katika familia ya watoto saba wa mzee Adrian Mganyo Mvungi aliyekuwa mkulima wa kawaida na mfugaji.

Hadi jana mchana, NIPASHE ilishuhudia namna familia ya Mvungi ilivyokuwa katika hekaheka za kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa kaburi atakalozikwa Dk. Mvungi, akiungana na wazazi wake wawili pamoja na kaka yake, ambao kwa sasa wote wametangulia mbele ya haki.

MIUNDOMBINU YA BARABARA
Barabara itakayotumika kuupitisha mwili wa Dk. Mvungi kutoka katika barabara kuu ya Moshi-Dar es Salaam kwenda nyumbani kwao, Chamakera, inapitika ingawa msafara wa waombolezaji pamoja na makundi mengine ya jamii yanayotoka nje ya Wilaya ya Mwanga wanapaswa kuwa makini kutokana na barabara hiyo kutokuwa katika hali nzuri.

Kufika Chamakera ni umbali wa takribani kilomita 11 kutoka barabara kuu kwenda katika uwanda wa juu wa safu za milima ya Upare, zenye miinuko mikali na baridi ya wastani nyakati za mchana.

Waombolezaji wanaotoka nje ya Wilaya ya Mwanga na Mkoa wa Kilimanjaro wanashauriwa kuwa na nguo za joto kwa ajili ya kujikinga na baridi kali nyakati za usiku kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa katika uwanda wa juu wa safu za milima ya Upare.

HALI YA USAFIRI

Hili ni eneo, ambalo linakabiliwa na shida ya usafiri wa mabasi ya abiria kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii, kwa hali hiyo wananchi wengi hulazimika kukodi usafiri wa pikipiki kutoka Kisangara hadi Kisangara Juu kwa Sh. 10,000 kwenda na Sh. 10,000 kurudi barabara kuu.
Chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment