UMOJA wa Wafanyabiashara wa Kariakoo, Dar es Salaam, umesema hauamini kama raia wa China wanaofanya biashara za Kimachinga wameingia nchini kwa kibali, vigezo na masharti ya kuendesha biashara za aina hiyo.
Kauli hiyo imekuja baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, MariaBilia, kusema kuwa raia yeyote kutoka nje ya nchi hazuiwi kufanya biashara ili mradi awe ametimiza vigezo na masharti na sheria za nchi.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam juzi, katibu wa umoja huo, Peter Kyando, alisema bado kuna haja kwa Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Viwanda na Biashara kutoa ufafanuzi kuhusu vibali na mikataba vya uingiaji wa raia hao.
Alisema kama raia hao wameruhusiwa kuingia nchini kwa ajili ya kufanyabiashara hizo ndogo ndogo ambazo Watanzania wanaweza kuzifanya, serikali inapaswa kutambua kuwa haikuwatendea haki wananchi wake, kwani hata China biashara kama hizo hakuna Mtanzania anayeruhusiwa kuzifanya.
Kyando alisema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wenyeji, wakidai biashara hivi sasa imewawia ngumu, ni baada ya raia hao wa China kujiingiza na kuzishika njia zote kuu za biashara katika eneo hilo la Kariakoo.
“Hatujui vibali vyao vimewaruhusu kufanya kazi gani hapa nchini lakini naamini kuwa viongozi wanaweza kuwa na majibu, ndugu zetu hawa wamekuwa wakifanya biashara hata zilizopaswa kufanywa na wajasiriamali wadogo wadogo,” alisema.
Kyando alisema inasikitisha kuwaona raia hao wa China waliodhaniwa kuwa ni wawekezaji wakubwa wakitembeza maua na barafu barabarani, wengine wakiuza sufuria, mifuko ya kike kwa bei ya reja reja
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment