Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameiagiza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhakikisha mchakato wa Sheria ya Usalama kwenye mitandao unakamilika na kuanza kutumika, ili kudhibiti wanaotoa siri za nchi kwa kisingizio cha uhuru wa habari.
Hayo aliyasema jana kwenye hafla ya uzinduzi wa mtambo maalumu wa usimamizi na uhakiki wa Mawasiliano ya Simu, (TTMS), iliyofanyika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) Dar es Salaam.
Rais Kikwete alisema hakuna nchi yoyote duniani ambayo haitunzi siri zake, kwa kuwajambo hilo ni muhimu kiusalama, hata kwa mataifa ambayo yamekuwa mstari wa mbele kutetea uhuru wa vyombo vya habari.
Alisisitiza kwa kumtolea mfano aliyekuwa Jasusi wa Marekani, Edward Snowden, anatuhumiwa kuvujisha siri za nchi hiyo kwenye mtandao, ambaye sasa amekimbilia mafichoni Urusi. Aliwapongeza TCRA kwa hatua hiyo, akieleza kuwa inawezesha uchumi wa nchi kupata kichocheo cha kukua kwa kuwa sasa kutakuwa na udhibiti wa mawasiliano hasa ya simu za nje ya nchi na kuongeza kipato kwa taifa.
Awali Mkurugenzi wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema kufungwa kwa mitambo hiyo, kunakwenda pamoja na kuwapo kwa kanuni mpya za mawasiliano ya usimamizi na uhakiki wa mawasiliano ya simu (TTMS, Regulation2013), ambapo imewezesha Serikali kupata senti 7 kati ya 25 zinazotozwa kwa kila dakika na nyingine zinagawanywa kwa kampuni husika.
“TCRA imefanikiwa kuilipa Hazina mgawo wa mwezi Oktoba, kwa mujibu wa Sheria ya TMMS Sh1.6 bilioni, leo tutakabidhi malipo ya Sh1.6 bilioni malipo ya Novemba hatimaye mwezi Machi tutalipa ya Desemba,” alisema Nkoma.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment