Tuesday 25 February 2014

TAHADHARI KWA WAREMBO WANAOKWENDA CHINA KUFANYA KAZI.


AMA kweli dunia hadaa, ulimwengu shujaa! Kumeibuka mchezo mchafu, kuna Watanzania wanawachukua warembo nchini na kuwapeleka China kwa ahadi kwamba wanakwenda kufanya kazi saluni, wakifika kule wanawanyang’anya paspoti na kuwauza kwa wanaume (ukahaba), sasa yamemkuta Mbongo aitwaye Sabrina au Habiba, Ijumaa Wikienda lina mkasa wa kusikitisha.

Habari za uhakika kutoka kwa chanzo chetu nchini humo zilisema kuwa, Sabrina (24), alifariki dunia Alhamisi iliyopita kufuatia kubakwa na wanaume watano, raia wa Nigeria ambao wamo nchini humo kibiashara.
Tukio hilo lilijiri kwenye hoteli moja iliyopo kwenye Mji wa Guangzhou ambao umejaa wageni wengi, wakiwemo Watanzania.

SIKU YA TUKIO
Rafiki wa karibu wa Sabrina, Saada alisema siku ya tukio, marehemu akiwa katika harakati zake za kutafuta wateja alikutana na Mnigeria mmoja ambaye walipatana kulala wote kwa usiku mzima.
“Kumbe yule Mnaigeria alikuwa na wenzake wanne. Usiku walimwingilia wote kwa nguvu kwa kumbaka mpaka akapoteza maisha palepale. Ni ukatili mkubwa.
“Wale watu walipogundua Sabrina amekufa waliuchukua mwili wake na kuutupa chini kutoka ghorofa ya tano,” alisema rafiki huyo.
MAITI YAKUTWA HAINA FIGO, MOYO
Habari zaidi zilidai kuwa mpaka juzi (Jumamosi) madaktari waliokuwa wakiuchunguza mwili wa Sabrina waligundua hauna figo na moyo, jambo linalozidi kuzua hofu juu ya muaji yake.
NI BIASHARA ILIYOIBUKA CHINA?
Ilidaiwa kuwa nchini China imeibuka biashara ya viungo mbalimbali vya binadamu ambapo ili vipatikane ni lazima mwenye viungo hivyo auawe kwa njia yoyote.
SABRINA AFA, MGANDA APOTEA
Mtoa habari wetu alisema wakati Wabongo wakiwa kwenye maombolezo ya kifo cha Mtanzania huyo, mrembo mwingine raia wa Uganda, nchi ambayo imo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki amepotea katika mazingira ya kutatanisha nchini humo.
Baadhi ya watu wana wasiwasi kuwa kupotea kwa msichana huyo kunahusiana na kushamiri kwa biashara ya viungo vya binadamu.
SABRINA ALIKWENDAJE CHINA?
Mwezi Julai, mwaka jana, Sabrina alikwenda nchini humo akidanganywa na mwanamke mmoja kwamba atapata kazi kwenye saluni ya wanawake lakini baada ya kufika alijikuta akiingizwa kwenye biashara ya ukahaba bila ridhaa yake mpaka alipokutwa na mkasa huo uliopoteza maisha yake.
TAHADHARI KWA WAREMBO WANAOKWENDA CHINA KUFANYA KAZI SALUNI
Imebainika kuwa, kumeibuka wimbi la Wabongo wanaofanya ‘uwakala’ wa kuwachukua wasichana wa Kitanzania kwa kuwadanganya kwamba wanakwenda kufanya kazi za saluni nchini humo.
Mara baada ya kufika, wasichana hao hunyang’anywa paspoti ili washindwe kuondoka nchini humo na kushinikizwa kujiuza (ukahaba) huku waliowapeleka wakipokea fedha kutoka kwa wateja.
KUIKOMBOA PASPOTI
Habari zilisema kuwa mhusika hurejeshewa paspoti yake baada ya malipo yake kwa ‘wakala’ kufikia dola za Marekani 8,000 (kama shilingi milioni 12), ndipo huachiwa ‘huru’ kuendelea na maisha yake.
Wengi wakishaachiwa hushindwa kurejea Bongo na kujikuta wakiendelea kuuza miili katika mahoteli na klabu huku wakikutana na majanga mbalimbali.
MASOGANGE, KAJALA NA DIDA
Watanzania waishio nchini humo wamewatahadharisha mastaa wa Bongo, wakiwemo Mtangazaji wa Radio TimesFM, Khadija Shaibu ‘Dida’, msanii wa filamu Kajala Masanja na Video QueenAgnes Gerald ‘Masogange’ ambao hupenda kwenda nchini humo kwa shughuli zao, kutokubali kuwa karibu na mawakala wa kuchukua wasichana Bongo kwa kuwadanganyia kazi ya saluni kwani wanaweza kujikuta pabaya siku moja.
DIDA
Ijumaa Wikienda lilimsaka Dida siku ya Jumamosi iliyopita na kumuuliza kuhusu kuwepo kwa mawakala hao ambapo alikiri kusikia huku akisema warembo wenyewe wanapaswa kuwa macho na udanganyifu huo.
“Najua wapo Wabongo wanaofanya shughuli hiyo, si China tu hata India, unapelekwa kwa ahadi ya kazi ya saluni, ukifika hamna cha saluni wala nini? Warembo wawe makini jamani, nenda China kama una uwezo wako mwenyewe kufanya ‘shoping’ lakini si kupelekwa,” alisema Dida.
BALOZI WA TANZANIA-CHINA
Juzi, Ijumaa Wikienda lilimtafuta Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali Mstaafu Abdulrahman Shimbo ili azungumze lolote kuhusu tukio la Sabrina, lakini simu yake ilionekana kutokuwa hewani kwa muda mrefu.
chanzo:globalpublishers

No comments:

Post a Comment