Tuesday 25 March 2014

Mmarekani adakwa na dawa za kulevya

Dar es Salaam. Kikosi cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, kimemtia mbaroni Raia wa Marekani, Kobina Danso (22) akiwa na kilotatu za dawa za kulevya aina ya Heroine.
Akizungumza jana, Kamanda wa Kitengo hicho, Kamishna Godfrey Nzowa alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 23 mwaka huu, saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA), akiwa tayari kuunganisha ndege kwenda Canada.
Kamanda Nzowa alisema mtuhumiwa huyo alikuwa anasafiri na ndege ya Shirika la Uswisi kuelekea Canada akiwa na hati ya kusafiria ya Marekani yenye namba 505416471.
Nzowa alisema mtuhumiwa huyo wa Ghana mwenye uraia wa Marekani, alikuwa anasafirisha dawa hizo zikiwa kwenye begi lake la nguo.
Alisema kikosi hicho kilimtilia shaka kabla ya kumpekua na kumkuta akiwa na ‘mzigo’ huo.
“Bado tunamhoji ili kubaini dawa hizo alikuwa anazipeleka kwa nani na tunataka tujue mtandao wake wote,” alisema Kamanda Nzowa.
Hivi karibuni, mkazi wa Buguruni, Mashusha Matata (30), alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akiwa na kete 102 za dawa za kulevya aina yaCocaine.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment