Wednesday, 9 July 2014
Kuna nini `nyuma ya pazia` la mabomu Arusha?
Ni rahisi kuamini kwamba jiji la Arusha lililo miongoni mwa vivutio muhimu vya utalii nchini, linaelekea kuchafuka kiasi cha kutishia uhakika wa usalama kwa wakazi wake na wageni wanaolitembelea, wakiwamo watalii wa ndani na nje.
Kuchafuka kwa jina jema na zuri la Arusha, kunatokana na matukio kadha wa kadha, lakini zaidi ni mfululizo wa mabomu yanayosababisha vifo, majeraha na uharibifu wa mali.
Kiasi cha matukio matano yanayohusiana na milipuko ya mabomu, yamerekodiwa kutokea jijini Arusha, yakihitimishwa na lile la usiku wa Alhamisi iliyopita lililotupwa na kulipuka nyumbani kwa kiongozi wa taasisi ya Answaar Muslim Youth Centre, Kanda ya Kaskazini, Sheikh Sudi Ally Sudi.
Yapo matukio kadhaa ya milipuko ya mabomu iliyotokea katika mikoa tofauti, Arusha ikishuhudia idadi kubwa miongoni mwa rekodi iliyopo.
Miongoni mwa maswali makuu ya kujiuliza hapa ni kwamba, kuna nini Arusha kiasi cha kusababisha mfululilzo wa matumizi ya mabomu dhidi ya binadamu na mali zao?
Je, vyombo vya ulinzi na usalama vinayatafakari matukio hayo, vinajipanga, vinaratibu na kutekeleza mkakati utakaoleta ufanisi katika kukabiliana na uovu huo?
Kwa hali ilivyo, kwingineo, hivyo tunaamini kwamba hata kwa hili la Alhamis iliyopita, hali inaweza kuwa hivyo.
Ndiyo maana hatutaki kuamini kwamba kwa weledi uliopo kwa vyombo vya ulinzi na usalama, si rahisi kuendelea kushuhudia milipuko ya mabomu Arusha vinginevyo, kama kuna kitu kimejificha ‘nyuma ya pazia’ ni vizuri kikafuatiliwa ili nuru ya matumaini katika kukabiliana na uhalifu huo ionekane na kuenea nchi nzima.
Ni vigumu kuamini kwamba vyombo vya ulinzi na usalama wanatimiza wajibu wao kwa kiwango cha kuridhisha, badala yake kuna kila dalili tunazoamini kwamba zinatokana na sababu kama ya uzembe.
Sisi tunaamini hivyo kwa sababu, ni vigumu kwa nchi iliyo na mfumo wa utawala unaotokea ngazi ya taifa hadi katika ngazi za msingi kwenye jamii, kushindwa kuwabaini wahusika wa vitendo hivyo na kuwachukulia hatua za kisheria huku ikijipanga kuyadhibiti yasitokee.
Vyombo vya ulinzi na usalama jijini Arusha vina wajibu mpana, kwa kushirikiana na umma, kuhakikisha kwamba tatizo la matumizi ya mabomu katika kuwashambulia, kuwajeruhi na kuwaua watu linafikia ukomo wake.
Kwa maana, haiwezi kukubalika kwamba watendaji wa vyombo hivyo, waliopewa dhamana ya kuhakikisha kunakuwapo amani, usalama na utulivu wa kudumu kwenye eneo hilo lililo miongoni mwa yanayotegemewa kwa ukuaji wa pato la taifa, wakashindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
Tunatambua kwamba matukio ya uhalifu hivi sasa ‘yanazingirwa’ na matumizi makubwa ya teknolojia kiasi cha kusababisha udhibiti wake kuwa mgumu.
Ingawa ni hivyo, asili ya uhalifu wa kutumia mabomu unaoendelea kukua nchini, hususani jijini Arusha haionyeshi ishara na dalili za kuwapo teknolojia inayoweza kuwashinda waliopo kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, kushindwa kuchukua hatua zinazostahili.
Inafaa sana kwa vyombo hivyo kurejea katika misingi na mafundisho yao, yakiwamo ya namna bora ya kuvitambua na kuvidhibiti vyanzo vyake kama ilivyo kwa mabomu yanayoendelea kuwaathiri raia wa Arusha.
Kuendelea ‘kuzembea’ na kushindwa kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti uhalifu unaotokana na matumizi ya mabomu, kunajenga mazingira ya kulichafua jina la Arusha, kiasi cha kufikia kuliweka katika orodha ya maeneo yasiyokuwa salama kwa wenyeji na wageni, wakiwamo watalii kutoka nje.
Ni kutokana na hali hiyo na umuhimu wa Arusha kwa nchi na watu wake, tunatoa wito kwa wahusika, wakiwamo wakuu wanaoshiriki uteuzi, usimamizi na ufuatiliaji wa watendaji katika vyombo vya ulinzi na usalama, kuchukua hatua madhubuti zinazolenga kuirejesha Arusha kuwa eneo lenye amani na usalama.
Kwa bahati mbaya, kila kunapotokea mlipuko ama aina yoyote ya uhalifu unaofanana na huo, jeshi la polisi na viongozi wengine wa serikali, wamekuwa wakitoa kauli za ‘tutawasaka wahusika popote walipo mpaka wapatikane na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.”
Tunasema kwa bahati mbaya inakuwa hivyo kwa sababu, hakuna hatua zenye kuleta tumaini la kupatikana kwa suluhu ya milipuko ya mabomu iliyowahi kutokea hasa jijini Arusha.
chanzo:nipashe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment