Mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, Mirerani, wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, Daud Madaha, amepigwa risasi kifuani na mchimbaji mdogo wa madini hayo na yuko mahututi katika Hospitali ya Rufaa ya Selian, jijini Arusha.
Tukio hilo lilitokea juzi, majira ya saa 11:00 jioni, katika moja ya baa maarufu iliyoko katika mji mdogo wa Mererani ijulikanayo kwa jina la Beach Boy.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Francis Mashue, alidai kuwa, Madaha alipigwa risasi kifuani na mmoja wa wachimbaji (jina tunalo), baada ya kudai kuwa (Madaha) amempa kiasi kidogo cha fedha.
Alisema baada ya mtuhumiwa kupewa fedha hizo, ghafla alitoa bastola na kumpiga Madaha kifuani, ambaye baada ya hapo alianguka chini huku akilalamikia maumivu.
Francis alisema watu waliokuwa katika baa hiyo walimkamata mtuhumiwa huyo na silaha yake na kumfikisha katika kituo cha polisi Mirerani.
Alisema baada ya hapo, walimchukua majeruhi huyo na kumkimbizia katika hospitali hiyo, ambako amelazwa na hali yake inaelezwa kuwa siyo nzuri.
Akizungumza kwa shida hosptalini hapo, Madaha alisema siku tatu zilizopita, mtuhumiwa huyo alimtishia kwa bastola na hivyo akalazimika kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mirerani.
Alisema mtuhumiwa huyo aliamriwa kukabidhi silaha hiyo polisi.
“Nilishangaa kumuona (mtuhumiwa) akiwa na silaha hiyo jana wakati ananipiga nayo, kwani siku tatu tu zilizopita aliamriwa kuikabidhi katika Kituo cha Polisi cha Mirerani baada ya kutishia kuniua,” alisema kwa tabu.
Madaha aliongeza kuwa, mara kwa mara mtuhumiwa amekuwa akiwatishia watu mbalimbali kwa kutumia bastola hiyo na wamekuwa wakitoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Mirerani, lakini cha kusikitisha ni kwamba hakuna hatua za maana zinazochukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo.
Akizungumzia hali ya majeruhi huyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Hosptali ya Selian, Dk. Paul Kisanga, alithibitisha kumpokea Madaha juzi, majira ya saa 2:30 usiku
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment