Siri ya kushambuliwa kwa basi la mahabusi jijini Dar es Salaam imefichuka, ikielezwa kuwa lilikuwa ni jaribio la majambazi kupora fedha kutoka kwenye gari ndogo iliyokuwa kwenye foleni karibu na basi hilo.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema kuwa majambazi hayo yalitaka kupora maeneo ya jirani na eneo la Hospitali ya Regency.
Nazo taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa majambazi hayo yalitaka kupora fedha kwenye gari dogo lililokuwa kwenye foleni na askari waliokuwa ndani ya basi la maabusu walipowabaini wakijiandaa kushambulia, majambazi wakaanza kushambulia basi hilo ili kujihami.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, jana akizungumza na waandishi wa habari, alisema majambazi hayo yalijihami kwa kushambulia basi hilo wakati yakitaka kutekeleza uhalifu wao.
Hata hivyo, Kamanda Kova hakufafanua kama kuna kiasi cha fedha kilichoporwa zaidi ya kuwataja majeruhi watatu ambao ni askari magereza mmoja, polisi na maabusu.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni CPL Dotto (33) askari polisi ambaye mkazi wa Tegeta Kanisani aliyejeruhiwa kwenye titi la kulia kwa risasi na amelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, SGT Musofe (39), dereva wa basi hilo na mkazi wa Segerea pamoja na Doreen Damian, mahabusi na mkazi wa Tegeta ambaye alitibiwa na kuruhusiwa.
Alisema jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano kukamatwa kwa kundi hilo la uhalifu.
Msemaji wa Jeshi la Magereza, Juma Ntagunama, akizungumza na NIPASHE, alisema majambazi hayo hayakulilenga gari la maabusi bali yalikuwa kwenye harakati za uhalifu.
“Tunaendelea na uchunguzi wa kina wa tukio hili, tulichogundua majambazi yalijiandaa kupora fedha kwenye gari dogo, walipomwamuru mwenye gari kufungua kioo, askari magereza waliona tukio hilo na kutaka kuanza kupambana nayo ndipo yalipojibu mashambulizi na kurusha risasi ovyo kwenye gari hilo,” alisema Ntagunama.
Alisema dereva wa gari dogo alipoamuriwa kutoa fedha, alionyesha kukahidi na kusogeza gari pembeni kulikokuwa na watu na wakati huo gari la Magereza lilikuwa linakuja na ndipo majambazi yalipoanza kulishambulia kama njia ya kujihami .
Wakati huo huo, Koplo Dotto wa kituo cha polisi Kawe, mwenye namba WP 4481, hali yake inaendelea vizuri Muhimbili.
Akizungumza na NIPASHE, Afisa uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaisha, alisema askari huyo alifikishwa hospitalini hapo akiwa na mahabusi ambaye alitibiwa na kuruhusiwa.
“Koplo Dotto alifikishwa hospitalini akiwa hajitambui ila kwa leo (jana) alikuwa anaweza kuzungumza,” alisema.
Shuhuda wa tukio hilo, alisema akiwa kwenye foleni ya gari kuelekea mjini katika barabara ya Mwai Kibaki, gari dogo iliyokuwa ikitokea Kawe kwenda Shoppers iliyodaiwa kuwa na fedha ilipofika eneo la Million Hairs Salon jirani Hotel ya Regency lilikwama kwenye foleni huku gari la mahabusi likiwa karibu nalo.
“Ghafla tulisikia milio ya risasi kama sita au saba, majambazi yakiwa kwenye pikipiki yalimfuata dereva wa gari dogo na kumwamrisha atoe fedha na alikubali kufanya hivyo,” alisema.
Alisema kwa vile gari la mahabusi ni kubwa waliona tukio lile na kuanza kujiandaa kujibu mashambulizi ndipo majambazi yaligeuza kibao na kuanza kulishambulia na kuondoka kwa kasi kwa kutumia pikipiki.
“Ilitisha sana na watu waoga kama mimi nilikimbia kujificha kwenye mtaro,” alisema shuhuda huyo.
chanzo:Nipashe
No comments:
Post a Comment