Tuesday, 31 May 2011

FFU, WANAFUNZI WAPAMBANA

ASKARI wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), jana walilazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya maandamano ya amani yaliyofanywa na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tosamaganga, walioandamana kwenda katika ofisi za mkuu wa mkoa wa Iringa kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya uongozi wa shule yao.
Tukio hilo lililowahusisha zaidi ya wanafunzi 1,000 lilitokea kati ya majira ya saa 4 asubuhi hadi saa 6 mchana baada ya polisi kufukuzana na wanafunzi hao kwa lengo la kuwatawanya pasipo mafanikio kutokana na wengi wao kukimbilia porini na wengine katika nyumba za wenyeji wa maeneo waliyokuwapo.
Hatua hiyo ilisababisha hali ya amani, kwa wananchi wa maeneo ya Mseke ambao kutokana na mabomu hayo walilazimika kuzihama nyumba zao na kukimbilia porini ili kuyakwepa mabomu hayo, kutoweka.
Waandishi wa habari ambao pia walikuwepo katika eneo hilo wakifanya kazi yao nao walizuiwa kuchukua habari hizo na askari polisi hadi wapate kibali kutoka polisi.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia askari polisi hao waliokuwa wakiongozwa na Mkuu wa  Polisi Wilaya ya Iringa (OCD) wakikabiliana na  wanafunzi hao.
Kabla polisi hawajafika eneo hilo wanafunzi hao kwa nyakati tofauti walisema sababu ya kufanya mgomo wa kutoingia madarasani na kutaka kuandamana unatokana na uongozi mbovu wa shule  hiyo usiozingatia haki za binadamu.
Waliyataka madai yao kuwa ni mfumo wa ufundishaji kutofuata taratibu na kanuni za ualimu, ukosefu wa vitendea kazi kama madawati na vitabu.
Mengine ni hatua ya makamu mkuu wa  shule hiyo kutumia nafasi yake kujinufaisha yeye binafsi badala ya  kusaidia kukuza kiwango cha elimu na  mengine.
Madai mengine ni kupewa chakula   kisichokuwa na ubora kama wanavyoelezwa  wazazi huku wakimtaka mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Iringa kutolea ufafanuzi kuhusu bajeti inayotengwa kwa shule hiyo kwa ajili ya chakula.
Madai mengine ni ubadhirifu  wa mali za shule pamoja na fedha nyingine wanazochanga na matumizi mabaya ya  fedha za shule yanayofanywa na mhasibu hivyo kuutaka uongozi  wa  shule hiyo kuweka  wazi matumizi ya michango yao mbalimbali ambayo  wamekuwa  wakichangia.
“Tunataka pia kujua kuhusu ‘Fund’ ya wasomi  waliosoma hapa Tosamaganga  inatumikaje na leo tunaiomba  Wizara ya Elimu, Mkuu wa mkoa wa Iringa, mkuu wa wilaya, mkurugenzi na ofisa  elimu  kufika shuleni hapa na  kuja kusikia kilio  chetu wanafunzi.”
Tanzania Daima ilipomtafuta kwa simu kamanda wa polisi mkoa wa Iringa, Evarist Mangalla, aligoma kutoa ushirikiano wowote kuhusu suala hilo kwa madai kuwa vyombo vya habari viliripoti tofauti habari ya kutekwa magari katika milima ya Kitonga.
Mkuu wa shule hiyo hakuweza kupatikana kuzungumzia madai hayo kutokana na kuhudhuria vikao mbalimbali  vilivyokuwa vikiendelea kati ya uongozi wa shule hiyo na vyombo vya dola. 

No comments:

Post a Comment