Wednesday, 5 October 2011

HATIMAYE CCM WAMELIPENDA TENA GAMBA LAO AMBALO ALILIVUA ROSTAM AZIZ, JIMBONI IGUNGA.


MATOKEO ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Igunga yaliyokipa ushindi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea wake, Dk. Dalaly Kafumu, yamezongwa na malalamiko na manung’uniko kutoka kwa wagombea wengine.
Dakika chache baada ya matokeo hayo kutangazwa, wagombea, makada na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF) walieleza kusikitishwa na mwenendo wa kampeni na uchaguzi wa jimbo hilo.   
Hatua ya vyama hivyo viwili vya upinzani kutoa madukuduku yao ilikwenda pamoja na ile ya mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye, aliyeshika nafasi ya pili kugoma kutia saini fomu za matokeo hayo.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo ambao ulizongwa na matukio ya vurugu, propaganda chafu za kupakana matope na udini wakati wa kipindi chote cha kampeni, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Protace Magayane alisema jumla ya watu walikuwa 171,077.
Hata hivyo kwa mujibu wa Magayane waliopiga kura juzi Jumapili wakati wa uchaguzi huo ni watu 53,672 na kwamba idadi halali ya kura zilizopigwa zilikuwa ni 52,487. Kura 1,185 ziliharibika.
Akisoma matokeo hayo, Magayane alisema mgombea wa CCM ambaye ni Kafumu aliibuka mshindi kwa kuvuna 26,484 ambazo ni sawa na asilimia 50.46.
Magayane alisema Kashindye wa Chadema alipata kura 23,260 ambazo ni sawa na asilimia 44. 32 akimuacha kwa mbali mgombea wa CUF, Leopold Mahona aliyepata kura 2,104 ambazo ni sawa na asilimia 4.01.
Mageyane alisema  mgombea Stevene Mahui (AFP) alipata kura 235, wakati Hassan Lutegeza (Chausta) alipata kura 182 Saidi Cheni (DP) alipata kura 76 huku John Maguma (SAU) na Hemed Dedu (UPDP) aliambulia kura 63.
“….kwa mamlaka niliyopewa kisheria kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, namtangaza Dk. Kafumu wa CCM kuwa mbunge wa Igunga. Igunga hoyeeeee!” alihitimisha Magayane.
 Akizungumzia uchaguzi huo, Magayane alisema mgombea wa Chadema (Kashindye) alikataa kusaini fomu za matokeo kwa madai ya kutoridhishwa nayo.
 “Wagombea wengine wote na mawakala wao wameyakubali matokeo isipokuwa wa Chadema aliyekataa kusaini… Baada ya kumpatiayale matokeo alipoyaona nafikiri amefadhaika, hakusaini.
“…Hata hivyo kukataa kwake hakubadilishi matokeo kwa sababu toka mwanzo tulikuwa naye kwenye harakati zote,” alisema Magayane.
Msimamizi huyo wa uchaguzi alisema walichelewa kuyatangaza matokeo hayo mapema zaidi kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kukwamisha kazi ya kusafirisha masanduku kutoka vituoni.
“Kwanza mvua imechelewesha kuletwa kwa vifaa hapa, ndiyo maana tulianza kuhesabu kura saa nne usiku. Pili ni huu mfumo wa ‘results management system’ tunatakiwa kupitia hatua zote. huwezi kufanya mkato hata hivyo hatujachelewa kwa sababu tume ilitupa hadi tarehe nne na sisi jana (Jumapili) ndo tumepiga kura naamini tumewahi,” alisisitiza.
Akizungumzia matokeo hayo, pamoja na kukiri kushindwa aliyekuwa mgombea wa CUF alilalamikia mazingira ya uchaguzi huo akisema hakukuwa na uwanja sawa wa ushindani kwa kuwa pesa ilitawala katika kumtafuta mwakilishi wa jimbo hilo.
“Watu wamechagua fedha hawakuchagua kiongozi. Sikati tamaa kwa sababu umri wangu unaniruhusu kugombea tena, ila ninachokiona ni elimu ya uraia iongezwe kwa hawa watu kwa vile wanapoteza dhima ya kumpata kiongozi mwenye sifa,” alisema Mahona.
Naye mratibu wa kampeni hizo upande wa CUF, Julius Mtatiro, alisema, “Nashukuru matokeo yametoka kama yalivyo. Tumejifunza kwamba kuna uchaguzi wa pesa ambao mwisho wa siku Watanzania watajikuta kwenye wakati mgumu.
“…Hatuwezi kuyapinga maamuzi ya wananchi. Tumegundua kwamba wapigakura wanauelewa mdogo. Nadhani kwa kiasi kikubwa hili limetuathiri. Palikuwa na propaganda za hapa na pale na wananchi wameaminishwa kwamba sisi CUF ni CCM B.
  “Lakini matokeo yametusikitisha kazi kubwa iko mbele yetu kwa upande wa demokrasia hatuwezi kushindana na CCM kugawa fedha kwa vile sera ya CUF hairuhusu hilo.”
Kwa upande wake, Ofisa Uchaguzi wa Chadema, Basil Lema, aliyaelezea matokeo hayo kuwa ni kielelezo cha mzaha unaoendelea kufanywa na CCM ambayo haiko tayari kufanya siasa za ushindani wa haki.
Akifafanua, Lema alivitupia lawama vyombo vya dola likiwemo Jeshi la Polisi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) kwa kucheza rafu zenye lengo la kuibeba CCM.  
 “Ili kuonyesha hatuko tayari kuona ushenzi huu, tunapinga matokeo haya kwa kwenda mahakamani. Huko tutapata jukwaa la kusemea vitu ambavyo tunavipinga,” alisema Lema.
Tofauti na ilivyokuwa kwa washindani wake, akizungumza kwa furaha, Dk. Kafumu alisema alikuwa akitarajia kupata ushirikiano kutoka kwa wagombea wenzake na wakazi wa Igunga katika kuleta maendeleo huku akiahidi kukutana nao.
 “Ninaahidi kwamba nitapenda tushirikiane. Nitafanya mkutano na wagombea wenzangu ili tuweze kuzungumzia maendeleo ya Igunga, kwa sababu maendeleo hayana chama. Ni kwa ajili ya wote,” alisema Dk. Kafumu.
Akiuzungumzia mwenendo wa kampeni, Dk. Kafumu alikiri kwamba ulikuwa si wa kirafiki kutokana na kutawaliwa na lugha chafu hususan zilizokuwa zikitumiwa na wapinzani wake.
 “Changamoto ya kwanza ni maji kwa vile wilaya yetu ni kame sana hivyo nitajitahidi kuhakikisha maji yanafika Igunga,” alisema Dk. Kafumu.

HALI KABLA YA MATOKEO

Awali kabla ya kutangazwa rasmi kwa matokeo hayo, kundi la vijana wa Chadema liliandamana kuelekea kwenye Ofisi za Mkurugenzi wa Wilaya ambaye ndiye Msimamizi wa Uchaguzi wakishinikiza kutangazwa kwa mshindi waliyedai kuwa ni mgombea wao.
Wakati ukiwa njiani msafara huo wa vijana ulipambana na wenzao wa CCM waliokuwa katika eneo la hoteli ya Peak yalipoibuka mapigano yaliyohusisha kurushiana mawe maeneo ya kubezana.

No comments:

Post a Comment