Monday, 23 April 2012

PAPIC KUIBURUZA YANGA FIFA!!!!


KOCHA wa Yanga, Mserbia, Kostadin Papic, jana aliwaaga rasmi wapenzi na mashabiki wa timu hiyo, akisema atafungasha virago vyake Aprili 26, huku akitishia kuishitaki klabu hiyo kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kwa kutomlipa mshahara wake.
Kwa mazingira hayo, Yanga wataikabili Simba hapo Mei 5, katika mechi ya mwiosho ya Ligi Kuu, wakiwa chini ya Kocha Msaidizi, Fred Felix Minziro.   
Akizungumza baada ya mechi ya jana ya Ligi Kuu dhidi ya Polisi iliyoisha kwa timu yake kushinda mabao 3-1, Papic alisema hadi anaondoka, anadai mshahara wa miezi miwili.
Papic alisema, kwa vile uongozi wa klabu hiyo umekuwa ukifanya hivyo licha ya kutambua ni kinyume cha mkataba uliopo baina yao, ataipigania haki yake na ikiwezekana hata kulifikisha jambo hilo Fifa.
Alisema, tangu asaini mkataba na Yanga, amekuwa mvumilivu sana, kwani amekuwa akilipwa nje ya muda, kitu ambacho kilimweka kwenye mazingira magumu, lakini anashukuru anaondoka huku mashabiki wakimpenda.
Papic ametoa shukrani kwa wachezaji ambao kwa kipindi chote alichodumu Yanga, wamekuwa wakimpa sapoti kubwa na kusema, anashukuru kuondoka Yanga kwa ushindi wa dhidi ya Polisi – mechi ambayo ilikuwa ya mwisho kwake. 
“Nawashukuru mashabiki wa Yanga, kwa sapoti yao wakati wote, naomba niwaage, hii ni mechi yangu ya mwisho, nitaondoka Aprili 26, asanteni sana kwa umoja na mshikamano wenu kwangu,” alisema Papic.
Kabla ya kutua Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2009, aliwahi kuzinoa timu za Orlando Pirates, Maritzburg United, Kaizer Chiefs za Afrika Kusini na Hearts of Oak ya Ghana.
Kocha huyo ameifundisha Yanga kwa awamu mbili tofauti kwani Januari mwaka jana, aliondoka akimpisha Sam Timbe kabla ya Mserbia huyo kurejea Oktoba mwaka huo kumrithi Mganda huyo.
Kuondoka kwa Papic ni kitu kilichotarajiwa hasa ikizingatiwa, mbali ya kwisha kwa mkataba wake wa mizei sita, pia misimamo ya kocha huyo ikiwemo ujasiri wa kutamka kitu kinachomkera, vimekuwa chukuzo kwa uongozi wa Mwenyekiti Lloyd Nchunga.
Miezi kadhaa iliyopita, Papic aliingia kwenye mvutano mkubwa na uongozi wa klabu hiyo, pale alipoweka hadharani ukata uliokuwa ukimkabili yeye na wachezaji wake hadi kushindwa kukodisha uwanja na kununua maji ya kunywa wakati wa mazoezi.
Ingawa jambo hilo lilikuwa ni dhahiri kwani wachezaji walisimama mazoezi kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola, jijini Dar es Salaam, viongozi wa Yanga wakajitetea huku wakishutumu kitendo cha kocha huyo kuanika mambo hayo hadharani bila kuwashirikisha.
Hata hivyo, baadaye ikabainika kuwa, fedha ambazo walipaswa kulipwa mshahara wachezaji, zilikwenda kwa Timbe kama malipo ya fidia ya kuvunjwa mkataba wake wa miaka miwili. 

No comments:

Post a Comment