Sunday 24 June 2012

MENEJA WA TAIFA STARS ATAKIWA KUJIUZULU!!!


MAKOCHA wa timu za soka za wanawake na wadau wa mchezo huo, wamemtaka Meneja wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, Furaha Francis, naye kufuata nyayo za aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa aliyejiuzulu.
Hayo yalibainishwa jana kwenye mkutano wa dharura wa kujadili marekebisho ya Katiba ya Chama cha Soka cha Wanawake Tanzania (TWFA), uliofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano wa Msimbazi Center jijini Dar es Salaam, ambapo wadau walijadili pia matatizo yanayoikabili soka ya wanawake, ikiwamo kufungwa kwa Twiga Stars na Ethiopia.
Twiga Stars iliyokuwa ikisaka walau ushindi wa bao 1-0 kutoka kwa Ethiopia kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ili kujitwalia tiketi ya kucheza fainali za Afrika (AWC) Novemba mwaka huu nchini Guinea ya Ikweta, wiki moja iliyopita ilifungwa bao 1-0, hivyo kuaga.
Wakizungumza kwa machungu kwenye mkutano huo wa jana, baadhi ya makocha waliunga mkono hatua ya Mkwasa kujiuzulu wakisema, amekawia kuchukua hatua hiyo kwani kiwango cha timu hiyo kimeshuka kwa kasi kwa siku za hivi karibuni, hivyo kuashiria kuna tatizo.  
Kwa upande wake Hamis Pondamali wa timu ya Sayari Queens, alisema kutokana na kiwango cha Twiga Stars, Mkwasa amestahili kuachia ngazi pamoja na Meneja wa timu hiyo, Furaha, kwa kushindwa kudhibiti matatizo yanayoikabili timu hiyo hadi wachezaji kushuka viwango.
Akifafanua zaidi, Pondamali alidai kuwa kuna baadhi ya viongozi wa timu hiyo wamekuwa wakishiriki kushusha viwango vya wachezaji kwa kuwafanyia vitendo vya usagaji, huku baadhi yao wakiwagombea wachezaji hao kwa ajili ya kuwasaga.  
“Baada ya Mkwasa kuachia ngazi, huyu Meneja Furaha anasubiri nini? Naye alipaswa kuondoka kwa sababu viwango vya wachezaji vimeshuka kwa kiasi cha kutisha bila wao kuchukua hatua,” alisema Pondamali akiungwa mkono na Kocha mwenzake, Rizik Shawa.
Shawa aliongeza kuwa, kwa mtazamo wake Mkwasa ni kama amechelewa kujiuzulu kwani timu hiyo imeshapoteza mwelekeo kutokana na matatizo yaliyopo huku yeye akiwa mbishi kufanyia kazi ushauri kutoka kwa makocha wenzake.
Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Juliana Matagi Yasoda, aliwataka wajumbe wa mkutano huo kufanya marekebisho muhimu yatakayosaidia soka ya wanawake kupiga hatua kuanzia ngazi ya chini hadi taifa.
chanzo:daima
                                           

No comments:

Post a Comment