Sunday, 17 June 2012

MWANAUME AOTA MATITI-WATANZANIA NAOMBA WANISAIDIE ILI TATIZO LINANIKOSESHA RAHA HASA MBELE YA WANAUME WENZANGU!!!


MWANAKIJIJI wa Magomeni wilayani Bagamoyo, Khamisi Tanga (46) ameota matiti kwa madai ya kutumia ya dawa za ARV’S zinazotumiwa na watu wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Akizungumza na waandishi wa habari waliokwenda wilayani humo kufanya utafiti kuhusu utekelezaji wa sheria ya ukimwi na Chama cha Waandishi wa Habari za Ukimwi (AJAT), Khamisi alisema alipatwa na mkasa huo miaka mitatu iliyopita.
Akisimulia namna alivyoanza kuugua, alisema awali aliona matiti yake yakiongezeka ukubwa kila kukicha, lakini hakujua kama lingeweza kuja kuwa tatizo kubwa kama lilivyo sasa.
Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, ilimbidi kwenda kliniki anayohudhuria kupata dawa na kuwaeleza manesi, ambapo walimjibu kuwa imesababishwa na dawa anazotumia, na hivyo kulazimika kukatizwa dozi hiyo na kupewa aina nyingine. 
Hata hivyo, Khamisi alisema pamoja na kubadilishiwa dozi, hakuna mabadiliko na kuongeza kwamba hivi karibuni alipewa dawa nyingine ambazo kati ya hizo kuna zile zilizomsabishia kukua matiti na tayari ameanza kupata maumivu aliyokuwa akipata awali.
Kwa mujibu wa Khamisi, ameshahangaika kupata matibabu hadi Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, lakini hadi leo hajapatiwa tiba stahili ya kumaliza tatizo hilo. 
 “Watanzania naomba wanisaidie kwa njia yoyote ile ili niondokane na hali hii, kwani inanidhoofisha sana na kunikosesha raha, hasa mbele ya wanaume wenzangu.
“Hapa ninavyoongea na nyie waandishi, nilipimwa hadi kansa na matiti ndiyo kama hivyo mnavyoyaona, yanaendelea kukua na huniuma sana, hasa wakati ninapolala,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kumuomba Rais Jakaya Kikwete kumsaidia ili arudi katika uanamume wake, kwa sababu hivi sasa maisha yake yanazidi kuwa magumu kwa vile hawezi kufanya kazi yoyote. Mtaalamu wa magonjwa, Dk. Dina Komakoma, akielezea sababu za kutokewa kwa hali hiyo kwa wagonjwa wenye maambukizi ya VVU, alisema ni jambo la kawaida japo hutofautiana.
“Wengine hujikuta wakinenepa au wakikonda sana, na hili la Khamis sio mtu wa kwanza kupatwa na hali hiyo,” alisema na kuongeza kwamba inapotokea mgonjwa akapata hali tofauti kama hiyo, anapaswa kusitishiwa dawa.
Anayetaka kumsaidia Khamis kwa namna yoyote ile, awasiliane na mwandishi wa habari hizi kwa simu namba 0713 062281.

No comments:

Post a Comment