Monday, 16 July 2012

JOKATE MWEGELO ZAIDI YA UNAVYOMFAHAMU!!


WENGI ukiwauliza kuwa wanamfahamu vipi Kojate Mwegelo, jibu lao litakuwa ni Mshindi wa pili wa Miss Tanzania mwaka 2006.
Wengine watakuambia ni Miss Temeke mwaka 2006 na pia Balozi wa bia ya Redds wa mwaka huo huo. Kuna kundi la watu watakujibu kuwa ni mrembo aliyefanikiwa sana katika medani ya urembo.
Majibu yote hayo ni sahihi, hata hivyo kuna mengi ambayo wengi hawayafahamu kuhusu mrembo huyu.
Jokate ana vipaji lukuki, vipaji ambavyo anasema ndivyo vinavyomuweka mjini.
Tofauti na urembo, Jokate ana uwezo mkubwa katika uigizaji wa filamu, kipaji chake katika kuigiza kimeonekana katika filamu ya ‘Fake Pastors’ ambayo alicheza kama mtoto wa mzee wa kanisa lakini hakuwa na maadili mazuri.
Mbali na kuwa na uwezo mkubwa katika kucheza filamu, Jokate pia ni Mwendesha shughuli mbali mbali, maarufu MC, kazi ambayo kwa mujibu wa mrembo huyu, inamsaidia kuongeza kipato chake.
Kwa kuonyesha kuwa ana vipaji vingi, mrembo huyo alishinda mchujo wa kuwania nafasi ya kuwa mtangazaji wa kituo maarufu cha televisheni cha Channel O cha Afrika Kusini mwaka jana.
Jokate anasema haikuwa kazi rahisi kwake kufanikisha mahojiano mbalimbali katika matamasha nchini humo ambapo alikuwa akihoji watu mbalimbali maarufu wakati wa ‘Red Carpet.’
 “Niliweza kuwahoji zaidi ya wasanii 200 na mahojiano yote yalikuwa moja kwa moja , nilianza kwa  kuogopa, lakini nilipiga moyo konde na kuendesha mahojiano hayo kwa ustadi mkubwa, najivunia kuwa Mtanzania wa kwanza kutangaza katika kituo hicho.” anasema Jokate.
 “Watanzania wengi wanajua kwa nini Afrika Kusini ipo juu kimuziki na hata katika fani nyingine mbali ya michezo, ni nchi ambayo ina watu maarufu wengi (celebrities), wote hawa kabla ya kuingia katika ukumbi, ilikuwa lazima wapitie kwangu na kuhojiwa, ilikuwa kazi kubwa ambayo imeweza kuniongezea uzoefu mkubwa katika fani ya utangazaji.” anasema.
Anafafanua kuwa kwa sasa bado ni  mtangaziji wa kituo hicho, ingawa hurekodi vipindi vingi kabla ya kurejea nyumbani kuendelea na shughuli zake nyingine.
Anasema kuwa utaratibu wa Channel O umemwezesha kuingia katika fani nyingine ya ubunifu wa mavazi ambapo kwa sasa ameibuka na staili mpya ijulikanayo kwa jina la Kidoti.
Maonesho ya mavazi
Jokate ameshiriki maonesho ya mavazi mawili makubwa mojawapo likiwa la Mitindo la Red Ribbon lililokuwa maalum kuchangisha fedha kwa ajili ya watoto waliothirika na ugonjwa wa Ukimwi chini ya  Taasisi ya Tanzania Mitindo House (TMH) iliyochini ya mwenyekiti, Khadija Mwanamboka.
Katika maonyesho hayo, Jokate pia alikuwa mmoja wa wabunifu wa mavazi ya asili ya Kitanzania yaliyotumia malighafi za Khanga na Vitenge.
 “Tunaweza kutumia malighafu za hapa hapa nyumbani kuvaa nguo nzuri, kinachotakiwa ni ubinifu tu, nina kipaji hicho na tayari wadau wameanza kunipongeza  kwa kazi nzuri niliyofanya,” anasema na kuongeza:
 “Nimeona mwanga katika maonesho ya mitindo japo fani hii bado haijawa na muamko mkubwa, lakini nimeweza kufanya  mambo makubwa kama haya.”
Jokate anawashauri vijana kujishughulisha ili kupambana na hali ngumu ya maisha na kuachana na mambo ambayo yanawapotezea muda.
chanzo:http://www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment