Wednesday, 25 July 2012

MOI YAELEMEWA ,WAGONJWA WALALA SAKAFUNI!!!


HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili, Kitengo cha  Taasisi ya mifupa (Moi),imeelemewa baada ya wagonjwa kufurika katika wodi na kusababisha wengi wao kulala chini na kwenye korido wakati wakipatiwa matibabu.
Mwananchi imeshuhudia baadhi ya wagonjwa katika taasisi hiyo, wakiwa wamelazwa kwenye sakafu  ndani ya wodi na wengine wakiwa kwenye korido za hospitali hiyo.

Moja ya wodi zilizoathirika na msongamano mkubwa wa ongozeko hilo la wagonjwa ni Wodi ya Sewahaji inayotumiwa na Taasisi ya Mifupa(Moi) pamoja na Hospitali ya Muhimbili.
Akizungumza na Mwananchi , msemaji wa Taasisi ya Moi, Almasi Juma alisema kufurika kwa wagonjwa katika kitengo hicho kumetokana na athari za mgomo wa madaktari uliomalizika katika siku za hivi karibuni.
“Katika kipindi cha mgomo wagonjwa waliopatiwa huduma walikuwa ni wa dharura pekee, na hivyo kupelekea kurundikano kwa wagonjwa wa kawaida,”alisema Almas na kuongeza:

“Kitengo hiki pia kinahudumia idadi kubwa ya wagonjwa wanaotokana na ajali, hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa  kujaa kwa wodi zetu pamoja na zile tulizopewa na hospitali ya Muhimbili”.
Almasi alisema, tatizo hilo la mrundikano wa wagonjwa  linaweza kuchukua muda kidogo mpaka athiri za mgomo ziishe ndiyo hali itatengemaa na kuwa ya kawaida.

No comments:

Post a Comment