Saturday, 21 July 2012

MTAALAMU WA ATOMIKI ASIMULIA ALIVYOELEA BAHARINI KWA SAA NNE BILA KUJUA KUOGOLEA: AJALI YA BOTI ZANZIBAR:Gunia liliniokoa,


WAKATI jitihada za kuopoa miili ya watu waliofariki dunia katika ajali ya meli ya MV Skagit iliyozama Jumatano wiki hii zikiendelea, walionusurika kwenye ajali hiyo wameeleza jinsi walivyokumbana na zahama, mmoja wao akiwa mkazi wa Micheweni Pemba, Makame Masoud Ali (18), ambaye alisema kilichomsaidia hadi alipookolewa ni kushikilia gunia kwa zaidi ya saa mbili akielea nalo baharini.
Mbali na Ali, mwingine ni mfanyakazi wa Tume ya Nguvu za Atomiki Arusha, Salome Mwambinge ambaye alisema: “Kuokoka kwangu ni miujiza ya Mungu.”
Mwambinge ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar alisema: “Sijui kuogelea, lakini nilikaa kwenye maji kwa saa nne. Nilichoka na kukakata tamaa, nikajiachia ili ikiwezekana nife, lakini nashangaa leo hii ni mzima.”
Mtumishi huyo Tume ya Atomiki ambaye alikuwa safarini kuelekea Pemba kikazi, alisema aliokolewa akiwa hajitambui... “Ninachokumbuka ni kwamba waokoaji walinifunga kamba shingoni nikapata maumivu makali, nikapiga kelele wakaniachia, nikatumbukia tena kwenye maji na baadaye walifanikiwa kuniokoa na kuniweka kwenye boti.”
Alisema wakati akiwa katika harakati za kujiokoa, aliwaona watu kadhaa wakiwa wamekufa wakiwamo watoto.
Kwa upande wake, Ali alisema baada ya meli kuzama na yeye kutupwa nje, aliona gunia na kulidaka. Anasema alilishikilia kwa zaidi ya saa mbili kabla ya kuonwa na vikosi vya uokoaji.
Abiria mwingine mkazi wa Bagamoyo, Hamisa Akida alisema meli hiyo ilizama ghafla na haikuwa rahisi kuwa na maandalizi ya kujiokoa: “Kwa jinsi meli hiyo ilivyozama ghafla haikuwa rahisi kujiokoa, kilichotokea hadi tukaokolewa ni mapenzi ya Mungu,” alisema.
Alisema hali alipookolewa alikuwa ameshakunywa maji mengi na kuishiwa nguvu... “ lakini nashukuru ni mzima.”

Waliopatikana jana
Wakati majeruhi hao wakieleza hayo, jitihada za vikosi vya uokoaji hadi jana zilifanikisha kupatikana kwa miili 68 na kati ya hiyo 16 ilitambuliwa.

Waliotambuliwa ni Husna Ali Hamis (34) na
Kulthum Haji Khamis (34) wote wakazi wa Bagamoyo na Sichana Pandu (45 wa Kilimahewa Zanzibar).
Wengine ni Nadra Maulid Mkubwa (17) wa Chumuni, Zanzibar, Mwanaidi Abdallah Ramadhani (21) wa Morogoro, Zubeda Jumanne Kwagaya (26- Meya),
Idd Masoud Omari (Miezi 7- Tomondo) Riziki Mohamed Idd (21- Fuoni Zanzibar), Mwanaisha Khamis Haji (75) na Amina Shabani Kibega (24) wote wa Jang’ombe, Zanzibar.
Pia wamo Laki Victor Kadoro (28- Mbagala, Dar es Salaam), Damas Leo Mlima (54- Shangani),
Halima Sharifu Abdala (21-Kigamboni, Dar es Salaam), Ali Juma Ali (44- Jang’ombe, Zanzibar),
Raya Ramadhani Hasani (2- Shakani) Mwanaisha Omari Juma (20- Bunju, Dar es Salaam) na Maryam Idd Omari Omari (25) Shakani.

Washindwa kutambua miili

Hali katika Viwanja vya Maisara, wanakohifadhiwa maiti jana kulikuwa na mkanganyiko baada ya wananchi wengi kushindwa kuwaona ndugu zao ambao walikuwa wamesafiri katika meli hiyo wakiwamo raia wa kigeni.
Maiti moja ya raia wa Kenya imetambuliwa na ndugu zao ambao hata hivyo, walisema wamechanganyikiwa kuhusu namna ya kusafirisha mwili kwenda kwao.
Mmoja wa ndugu, John Mumee alisema wameitambua maiti ya ndugu yao aitwaye Martina Masela... “Lakini hatujui tutaisafirisha vipi kwenda Mombasa kwa sababu hatuna fedha, lakini pia hatuelewi tutasafirisha kwa njia gani kwa sababu mashirika ya ndege hayataki kusafirisha maiti.”
Alisema marehemu alikuwa akisafiri na mumewe, Bernard Kalii kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar wakiwa na ndugu mwingine, Mary Kioko ambao bado hawajapatikana.
“Tumepata maiti hiyo moja lakini wenzake wawili bado hatujawapata, hatuelewi tufanye nini hapa tumechanganyikiwa tunaomba msaada wa haraka,” alisema Mumee.

No comments:

Post a Comment