WAZIRI wa Uchukuzi Dk, Harson Mwakyembe, amesema Oktoba mwaka huu, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wataanza kutumia usafiri wa reli.Mwakyembe alisema hayo juzi Dar es Salaam baada ya kutembelea Karakana ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), na kukagua maendeleo ya mradi wa usafiri wa reli ndani ya Jiji.
Katika ziara hiyo, waziri huyo pia aliagiza watu waliojenga ndani ya meta 15 kutoka katikati ya reli kuondoka mara moja.
Waziri huyo alisema vinginevyo wakati ukifika, nyumba za maeneo hayo zitavunjwa kwa nguvu na kwamba wamiliki wake hawatalipwa fidia.
“Nikifika bungeni Dododoma nitalizungumzia suala hili kwa sababu nimeshuhudia wazi watu wakiwa wanaishi katika maeneo ambayo hayastahili. Wengine wamefikia hatua ya kulima mazao mbalimbali karibu na reli, jambo ambalo ni la hatari kwa usalama wao,” alisema.
Alisema tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam litamalizika Oktoba mwaka huu baada ya kukamilika kwa ukarabari wa mabehewa na reli kutoka Ubungo Maziwa hadi Stesheni.
Dk Mwakyembe alisema Serikali imelazimika kutumia fedha za ndani kukarabati mabehewa na reli, ili kuharakisha mkakati wa kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
“Serikali imeamua kufanya matengenezo ya mabehewa na ukarabati wa reli kuanzia Ubungo Maziwa hadi Stesheni ili kupunguza kama si kumaliza kabisa tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaa na kuruhusu shughuli za kiuchumi kuchukua nafasi ,” alisema Dk Mwakyembe.
Alielezea matumaini yake kuwa kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi tatizo la msongamano wa magari litakwisha kabisa hasa kwa kuzingatia kuwa kuna mradi wa magari yaendayo kasi.
Alisema ingawa Serikali inaendelea na jitihada hizo, lakini inakwazwa na tatizo la kukosekana kwa mali pa kuegeshea magari.
“ Sawa tunafanya jitihaza za kupunguza au kumaliza kabisa tatizo la msongamano wa magairi jijini Dar es Salaam, lakini kuna changamoto ya kukosekana kwa sehemu za kuegesha magari,” alisema.
chanzo:http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment