Tuesday 23 October 2012

HAUSIGELI ATUMBULIWA TUMBO, ATOROSHWA, KISA MUME WA MTU

BINTI aliyekuwa akifanya kazi za ndani (hausigeli), Angel Lema (22) mkazi wa Leganga, Kata ya Usa River wilayani Arumeru, aliyetumbuliwa tumbo kwa madai ya kufumwa na mume wa mtu, ametoroka wodini katika hospitali alipokuwa amelazwa.
Tuhuma za tukio hilo zimethibitishwa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Meru, Dk. Azizi Msuya wakati akiongea na gazeti hili na kueleza kuwa awali binti huyo wakati akiletwa katika hospitali hiyo ilielezwa kuwa alijichoma kisu mwenyewe.
Alisema kuwa baadaye iligundulika kuwa binti huyo alichomwa kisu na mke wa bosi wake ambaye polisi bado wanaendelea kumtafuta baada ya kubainika kuwa alisuka njama za kumtorosha hospitalini majeruhi huyo.
Hata hivyo, Dk. Msuya alibainisha kuwa tukio hilo linawahusisha pia baadhi ya polisi wasio waadilifu ambao walishirikiana na watuhumiwa kumtorosha msichana huyo hospitalini ili kuficha ushahidi wa tukio hilo.
Dk. alieleza kuwa msichana huyo baada ya kufikishwa hospitalini hapo alikuwa katika hali mbaya huku utumbo ukiwa nje kutokana na jeraha kuwa kubwa,walipomhoji alikana kuchomwa kisu na mke wa tajiri yake.
Aidha, alisema wakati wakiendelea  kumfanyia matibabu ndipo baadhi ya ndugu walijitokeza na kubainisha kwamba binti huyo alichomwa kisu na mke wa tajiri yake baada ya kuhisi alikuwa akimwingilia kwenye mapenzi ya mumewe.
Dk. Msuya alilalamikia kitendo cha mgonjwa wake kutoroshwa akiwa chini ya ulinzi wa polisi. 
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas alipoulizwa juu ya tukio hilo alithibitisha kupokea taarifa hizo na kudai kuwa ametoa maagizo kuwa msichana huyo asakwe.
chanzo:http://www.globalpublishers.info

No comments:

Post a Comment