Monday 29 October 2012

WANACHAMA WA CCM NA CHADEMA WACHALAZANA MAPANGA NA FIMBO!!!!

Mtaa wa Lihumbu, Kata ya Mletele, Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, juzi uligeuka uwanja wa vita, baada ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupigana kwa mapanga na fimbo na kusababisha zaidi ya watu watano kujeruhiwa.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 9:00 alasiri wakati wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata ya Mletele.
          
Ilielezwa kuwa baada ya mkutano huo kufungwa, wafuasi wa Chadema akiwamo Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Chiku Abwao, walivamiwa na wafuasi wa CCM waliofika eneo hilo wakiwa katika gari dogo.

Habari zaidi zilifafanua kuwa baada ya wafuasi wa Chadema kuvamiwa, walianza kupigana na baadaye wafuasi hao walifanikiwa kulikamata gari dogo la lililokuwa limewabeba wafuasi wa CCM akiwemo Mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya hiyo, Paul Mangwe.

Inadaiwa kuwa ndani ya gari hilo, kulikuwa na mapanga 30, vipande tisa vya nondo, mundu nne, fimbo za mianzi nane na ndege mmoja aina ya bundi akiwa hai.

Mmoja wa wafuasi wa Chadema, Frank Mgao, alidai kuwa baada ya kukamatwa kwa gari hilo, polisi waliongozwa na Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo, Nico Mwakasanga, waliwakamata na kuwapeleka Kituo Kikuu cha Polisi cha Songea ambako wanaendelea kuhojiwa.

Mgao alisema baadhi  ya wanachama wenzake na wanachama wa CCM, wamejeruhiwa kwa kupigwa na mapanga sehemu mbalimbali za miili yao na wengine wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma kwa matibabu zaidi.

Kwa upande wake, Abwao aliiambia NIPASHE kuwa wakati wanachama wa Chadema walikifunga kampeni kijijini Lihumbu, walipata taarifa kuwa kuna kundi la wana-CCM wanapita kugawa fedha kwa wapiga kura, jambo ambalo liliwafanya kuanza kufuatilia ukweli wa jambo hilo.

Alieleza kuwa wakiwa wamesimama wakijadili suala hilo, ghafla waliliona gari dogo likiwa limebeba wafuasi wa CCM na nyuma yake likifuatiwa na gari aina ya Land Cruser lililowabeba wanachama wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Gerald Mhenga.

Alisema wanachama hao walisimamisha magari yao na kuanza kuwashambulia kwa nondo, mapanga na fimbo za mianzi.

Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Silim Mohamed, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alithibitisha kupigwa kwa wanachama wa Chadema.

Hata hivyo, Mohamed, alidai kuwa walifanya hivyo baadaya wafuasi wa Chadema kutaka kumteka mgombea udiwani wa CCM wa kata hiyo, Maurus Lungu.

Waandishi wa habari walikwenda katika Hospitali ya Mkoa Ruvuma na kuwawakuta baadhi ya majeruhi wa tukio hilo wakiwa wamelazwa hapo.

Baadhi ya wauguzi wa hospitali hiyo ambao walidai si wasemaji, walithibitisha kupokea majeruhi ambao baadhi yao wamelazwa wodi namba mbili na wengine walitibiwa na kuruhusiwa.

Waliwataja majeruhi waliolazwa kuwa ni Nyenje Ally Mponji (32), mkazi wa eneo la Ruvuma ambaye alipigwa na kitu chenye ncha kali kichwani, miguuni na mikononi, Mashaka Mbawala (45), mkazi wa Lizaboni, aliyepigwa na kitu chenye ncha kali kichwani na Thabit Selemani (29), mkazi wa Ruvuma, aliyejeruhiwa kichwani, mdomoni na mikononi na Mwenyekiti wa Chadema wa mtaa wa Changarawe kata ya Mletele, ambaye ana uvimbe kifuani aliodai umesababishwa na kupigwa na fimbo za mianzi.

Jitihada za kuwapata viongozi wa CCM wa wilaya hiyo ili kutoa ufafanuzi wa tukio hilo, ziligonga mwamba baada ya kutopatikana kwenye simu zao za mkononi.

Inadaiwa kuwa katika tukio hilo, kuna watuhumiwa ambao ni wafuasi wa Chadema na CCM wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Deusdedit Nsimeki, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Hata hivyo, Kamanda Nsimeki, alisema vurugu hizo hazikutokea kwenye mkutano wa kampeni.

Alisema chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na watu sita walijeruhiwa na wengine walitibiwa na kuruhusiwa kwenda makwao.

Hata hivyo, Kamanda Nsimeki, alikataa kuzungumzia tukio hilo kwa undani kwa maelezo  kwamba kwa sasa (jana), kulikuwa kuna 'tension' ya uchaguzi, hivyo polisi wanasimamia kwanza kazi hiyo.

"Tutaendelea na upelelezi baadaye, lakini tukio halikutokea kwenye mkutano; lilitokea pembezoni kabisa. Tulikamata watu wanne na tuliwahoji na kwa sababu ni majeruhi, tutawahoji baadaye, bado tunataka kwanza hii `tension' ya uchaguzi ipite," alisema.

Kata ya Mletele ni moja ya kata 29 ambazo juzi zilifunga kampeni za uchaguzi mdogo. Katika Kata hiyo, CCM imemsimamisha Lungu anayechuana vikali na Leocado Mapunda, wa  Chadema.

Uchaguzi huo mdogo unafanyika kwa lengo la kuziba nafasi iliyoachwa wazi baada ya aliyekuwa Diwani wa kata hiyo, Flavian Tamaambele (CCM) kufariki dunia.

DODOMA HALI TETE


Mkoani Dodoma, wakati zoezi la uchaguzi likifanyika kwa utulivu katika kata ya Msalato mjini hapa, kada wa Chadema, Batholomew Peter, amejiruhiwa baada ya kucharangwa mapanga na watu wanaodhaniwa kuwa ni wanachama wa CCM.

Akizungumza jana katika wodi namba moja ya Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Peter alisema alikumbwa na mkasa huo juzi saa 3:00 usiku katika kata ya Msalato alipokuwa akirudi  kumsindikiza mwanachama mwenzake.

Kata ya Msalato jana ilifanya uchaguzi baada ya Diwani aliyekuwapo kufariki dunia. 

Wagombea katika uchaguzi huo ni Nsubi Bukuku (Chadema) na Ally Mohamed (CCM).

Akizungumza kwa shida, Peter alisema alipokuwa akirudi, alitegeshewa kamba katika barabara, hali iliyomfanya kushindwa kuimudu pikipiki na hivyo kuanguka chini.

Alisema akiwa chini, alivamiwa na kundi la watu aliodai kuwa ni wanachama wa CCM na kumcharanga mapanga yaliyomfanya apoteze fahamu.

Kada huyo aliumizwa vibaya kichwani na mkononi na kulazimika kushonwa nyuzi 13 katika kidole baada ya kukatwa kwa mapanga.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM kata ya Msalato, Andrew Mdumula, alisema wanachama wa Chadema walikuwa wakipita katika nyumba za watu kwenye kata hizo kufanya vurugu.

Alikanusha majeruhi huyo kukatwa mapanga na wanachama wa chama chake.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani humu, Stephen Zelothe, alisema bado hajapata taarifa za tukio hilo.

Umejengeka utamaduni wa uhalifu kwa wafuasi wa vyama vikuu vya siasa nchini vya CCM na Chadema kupigana wakati wa kampeni, hali ambayo imesababisha majeruhi na hata vifo kama ilivyotokea Igunga, Arumeru Mashariki na Singida.

chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment