Wednesday 28 November 2012

King Majuto amlilia Sharo Milionea

                                           Mzee majuto na sharobaro milionea

                                        Sharobaro milionea
KIFO cha msanii Hussein Ramadhan ‘Sharo Milionea’ kimemshutua msanii mwenzake King Majuto hadi akaanguka na kupata shinikizo la damu.

Majuto alipatwa na hali hiyo baada ya kupata taarifa za msiba huo na hadi anazungumza na gazeti hili, ingawa alikuwa na nafuu, mwili wake ulikuwa umevimba.

Akizungumza na Mwananchi Majuto alisema: “Kimeniuma sana kifo cha mwanangu Sharo.
“Nimeshirikiana naye kwa mambo mengi, nilifahamiana naye tangu mwaka 2009 tulikutana pale Vijana Production, na tangu nimefahamiana naye, kuna mambo mengi sana tumefanya,” alisema Majuto ambaye mara baada ya kupata taarifa ya kifo cha msanii huyo alipata na shinikizo la damu.

“Nilimuongoza kwenye mambo mengi na siku zote nilikuwa nikimsihi asikimbilie kuoa kama walivyo vijana wengine ambao wakipata hela kidogo wanachokimbilia ni kuoa.
“Nilikuwa ninamwambia jenga maisha yako kwanza, hakikisha unakuwa na nyumba, gari na miradi, ili hata ukioa mtoto asipate shida nashukuru alinisikiliza alianza kupata mafanikio kifo ndo kimemchukua.

“Sijui nisemeje kifo kina siri nzito, ningejua anakufa lini ningekata rufaa na hata kutoa rushwa lakini hiyo ni siri ya Mungu pekee...alikuwa ameanza kupata mafanikio masikini, sijui ni macho mabaya ya watu, sijui Mungu pekee ndio anajua kwa sababu alikopatia ajali wala hakukuwa na kona kali.

“Alikuwa meneja wangu, matangazo yote mnayoyaona yeye ndio alikuwa akiingia mikataba yote na fedha zote, hakuwa mdhulumishi, kazi zote tulizofanya pamoja na yeye ndio alikuwa akisimamia, akiniambia mzee tusifanye hii kazi nami sifanyi.

“Alikuwa ana msimamo wake, akisema Sh1milioni ni hiyo hiyo habadiliki tofauti na mimi na roho ya huruma, nikimtajia mtu bei akiniomba basi napunguza, sifanyi hivyo kwa njaa, hapana, ila ni ile imani niliyonayo sasa tofauti na Sharo.

“Sidhani kama pengo lake kwangu litazibika na sijui kazi zangu nitazifanyaje tena bila yeye, alikuwa ni kila kitu kwangu pamoja na kumzidi umri.”
Mwenyekiti Simba
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage alitoa pole kwa wadau wa filamu na kumuelezea marehemu Sharo Milionea kuwa hakuwa msanii wa kawaida kwani ni miongoni mwa kizazi kipya cha vijana wa Kitanzania walioamua kutafuta maisha kwa kutumia vipaji walivyopewa na Mungu.

Yeye alijitumbukiza zaidi katika uchekeshaji na baadaye akaonyesha uwezo mkubwa katika fani ya muziki.
Maisha ya Sharo Milionea
Kila kona za miji na vitongoji vyake nchini, huwezi kukosa kusikia watoto wakisema ‘umebugi meen...nataka kula meen’ na yote hiyo ni staili na ubunifu wa msanii huyo.

Sharo Milionea aliyejizolea umaarufu kwa staili yake ya utembeaji na uongeaji, na aliwateka mashabiki wa vichekesho hususani vijana na watoto kutokana na kubuni staili yake ya kuiga madoido ya watu wa Marekani, na kujiweka katika maisha ya juu ambayo kwa hakika hawezi kuyafikia.

Ingawa aliigiza maisha hayo yeye binafsi hakupenda kabisa staili hiyo ya maisha na lengo la kuigiza ni kuwafundisha wenye tabia kama hizo kuacha, kwani binadamu wote ni sawa na hakuna aliyebora kuliko mwingine.

Alizaliwa Septemba 12, 1987 Muheza, Tanga. Alijiunga na Shule ya Msingi Lusanga na baadaye akasoma Sekondari ya Kwabutu, Tanga.
Alipomaliza shule mwaka 2005, alihamia jijini Dar es Salaam kumfuata mama yake aliyekuwa akiishi jijini kwa muda mrefu.
Sharo Milionea alianza kujiingiza katika sanaa tangu akiwa shule ya msingi mkoani Tanga, alipoingia jijini Dar es Salaam hapo ndipo kipaji chake kilipozidi kukua baada ya kukutana na muigizaji mkongwe, Mzee Majuto na kujiingiza moja kwa moja katika kundi la Vituko Show.

Baada ya kukaa kwa miaka kadhaa ndani ya kundi hilo hatimaye Januari 2012 Sharo Milionea alijitoa na kujiunga na kampuni ya Al-Riyami, iliyowafadhili kama kikundi cha vichekesho, chenye maskani yake mjini Tanga.

Kundi hilo lilikuwa likiandaa vipindi kwenye vituo mbalimbli vya televisheni hapa nchini na matoleo mbalimbali ya vichekesho kwenye CD na DVD ambazo husambazwa mitaani.
Sababu za kimsingi za Hussein Ramadhani kujiengua katika kundi la Vituko Show ni kukosa muda wa kufanya muziki kutokana kukaa kambini kwa takribani miezi sita huku akiamini atakuwa anakosa fedha nyingi wakati ana kipaji.
Hata hivyo, Sharo Milionea aliweka wazi sababu zilizomfanya ajiengue kundini na kuingia mtaani kuendeleza vipaji vyake katika uigizaji na kuimba , kuwa “Vinamlipa haraka tofauti na uigizaji pekee”.
Katika muziki, Sharo Milionea ambaye alikuwa na ratiba ya kufanya shoo za hivi karibuni katika maeneo mengi nchini, hivi sasa alikuwa anafanya vizuri katika wimbo wake wa ‘Chuki’ aliomshirikisha msanii Dully Sykes na ‘Changanya’ aliomshirikisha Ali Kiba.
Msanii huyo amefariki kabla ya kukamilisha albamu yake ya kwanza ambapo kwa mujibu wa prodyuza wake, Charles Kanjenje alikuwa akitarajia kuikamilisha mwanzoni mwa mwaka ujao kupitia studio ya Kiri Records.Kanjenje alisema kabla ya msanii huyo kukutwa na mauti, Januari mwakani alipanga kuendesha shindano la kuwasaka wasanii chipukizi watakaorithi na kuendeleza staili ya muziki wake alioubatiza jina la ‘Kupedekalee’.Wakati wa uhai wake alipofanya mahojiano na gazeti hili, Sharo Milionea aliwahi kusema kuwa jina lake linatokana na staili yake ya kuigiza kama Sharobaro, yaani mwanaume bishoo lakini milionea ni jina ambalo aliona ajiite mwenyewe kwa sababu ya vipaji alivyonavyo.
Aliwahi kusema pia kuwa anaweza kuchekesha, kuigiza filamu za kawaida, kuimba na kutumika kwenye video za wasanii wengine kwa makubaliano maalum.
Msanii huyo aliwahi kukiri wazi kuwa asingeweza kufika mahali alipofikia kimafanikio lakini hilo liliwezekana kwa msaada wa wasanii wengine, akiwemo Mzee Majuto na Kitale na kwamba watu hao walichangia kwa kiasi kikubwa kumfikisha hapo alipo.
Baadhi ya nyimbo alizowahi kufanya ni pamoja na ‘Sondela’ na ‘Hawataki’ alizoshirikiana na Rich Mavoko pamoja na Kanali Top zilifanikiwa kumuweka katika nafasi nzuri katika chati za muziki.Itakumbukwa Sharo Baro alinusurika katika ajali nyingine Januari 5 mwaka huu baada ya basi alilokuwa akisafiria la Taqwa kutoka nchi jirani ya Burundi kupata ajali katika eneo la Mikese mkoani Morogoro, akirejea Dar es Salaam.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment