Jumuiya ya Wasambaziji vyakula Zanzibar (ZESA) imesema vurugu za kikundi cha uamsho zimeshusha biashara za kusambaza vyakula na vinywaji kwenye mahoteli na migahawa inayohudumia watalii.
Katibu wa ZESA Twaha Mohammed Mburusi, alisema katika mahojiano na NIPASHE Jumapili yaliyofanyika Zanzibar jana.
Alisema utoaji huduma hizo kwenye vitega uchumi vya utalii imeathirika kwa asilimia 35 tangu kutokea vurugu hizo mwezi uliopita.
Kadhalika hali hiyo imeathiri wavuvi, wafugaji, wakulima na wafanyabiashara visiwani hapa na kwamba yote yametokana na idadi ya watalii kupungua kwa kuogopa vurugu hizo.
Aliongeza kuwa wawekezaji wamepunguza kiasi vya vyakula vinavyopokelewa kutoka kampuni 130 za kusambaza huduma hiyo katika vitega uchumi vya kitalii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Chura General Supplies Mussa Yussuf Chura, aliunga mkono maelezo hayo akiongeza kuwa kiwango cha usambazaji wa vyakula na vinywaji mahotelini kimeshuka.
Alisema msukosuko kwenye sekta ya utalii pia utaathiri kwa kiwango kikubwa wakulima , wafugaji wafanyabiashara na wajasiriamali wanaotegemea sekta hiyo .
Alionyesha wasiwasi kuwa msukosuko huo wa sekta ya utalii pia utawaumiza wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania Bara wanauza katika soko la utalii la Visiwani .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar, (ZATI) Abdul Samadu, alisema jumuiya hiyo itafanya utafiti kufahamu ukubwa wa athari za vurugu hizo.
Lakini alisema si maeneo yote ya ukanda wa utalii yaliyoathirika na vurugu hizo zilizotokea baada ya kiongozi wa Uamsho Sheikhe Farid Hadi Ahmed (41) kudaiwa kutoweka kitatanishi kisha kuonekana tena Oktoba 20 mwaka huu.
Sekta ya utalii inachangia asilimia 25 ya pato la taifa na asilimia 83 ya fedha za kigeni pia ikiwa imeajiri watu 12,000 huku pia ikinufaisha wavuvi , wafugaji na wakulima.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment