Friday, 9 November 2012

Uzushi wa wagoni wazua hekaheka Dar!!!!



                                 Wananchi walio enda kushuhudia ugoni


                                 Polisi wakiwasambalatisha wananchi
HEKAHEKA ya aina yake, ilitokea jana kwenye Hospitali ya Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, baada ya kudaiwa kuwapo na watu waliokuwa wamefanya uzinzi na kushindwa kutengana.
Tukio hilo lililozusha sintofahamu, lilidaiwa kutokea kwenye nyumba moja ya kulala wageni (jina tunalo) iliyopo Temeke na wahusika walipoona wanashindwa kujinasua baada ya kumaliza haja zao, waliomba msaada wa kufikishwa hospitalini hapo.
Habari hizo zilizoanza kuenea majira ya asubuhi zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii na mikoa mbalimbali jambo lililosababisha baadhi ya wasomaji kupiga simu katika chumba cha habari kutaka kujua nini hasa kilichotokea.
Mashuhuda wa tukio hilo, waliliambia Mwananchi kuwa watu hao walifikishwa hospitalini hapo wakiwa kwenye gari aina ya Canter kwa ajili ya kupatiwa huduma baada ya kila mmoja kumng'ang'ania mwenzake huku wakiwa wamejifunika shuka za nyumba hiyo ya kulala wageni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime alipofuatwa kuzungumzia tukio hilo lililotokea mita takriban 300 kutoka ofisini kwake, ilielezwa kuwa yuko kwenye kikao.
Hata hivyo, alipotafutwa baadaye jioni alisema: “Habari hizo ni uongo, hazina ukweli wowote, na polisi imeanza uchunguzi kufahamu nani aliyeanzisha uvumi huo.”
Kwa mujibu wa Kamanda Misiime, ambaye anahamia Dodoma kuchukua nafasi ya Kamanda Zelothe Steven anayestaafu, alisema polisi wanaendelea na doria hadi hapo hali itakapotengemaa katika hospitali hiyo.

Kinachodaiwa kutokea Hospitali ya Temeke
"Muda wa saa 4:00 asubuhi liliingia gari aina ya Canter hospitalini huku likiwa na watu wawili ambao walifunikwa shuka na kupelekwa katika ofisi zilizopo kwenye jengo la kuhifadhiwa maiti," alisema mmoja wa mashuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Khamis Ramadhani.
Alisema: "Habari hizi zilienea kwa kasi na kuvuta hisia za wengi na walifika hospitalini hapo kwa ajili ya kuwashuhudia watu hao.
"Baada ya kutokea hali hiyo, Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU)  walifika kwa ajili ya kuwatawanya baada ya kuanza ghasia huku wengine wakitumia nafasi hiyo kupora mali kwa watu wengine."
Mwandishi wa habari hizi, alishuhudia Polisi ikiwatangazia watu kuondoka eneo hilo vinginevyo watatumia nguvu.
Baada ya watu kutotii amri ya kuondoka, polisi hao walianza kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya watu hao.
Hata hivyo, watu hao waliondoka eneo la tukio, lakini baadaye walirudi tena na askari  kulazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Baada ya kuona hali inazidi kuwa ngumu, uongozi wa  hospitali hiyo ulifunga milango na kuzuia watu kuingia ndani wakiwamo wagonjwa wa nje waliofika kwa ajili ya kutibiwa.
Habari ambazo Mwananchi lilidokezwa baadaye na mmoja wa askari waliokuwa wakifanya kazi ya kutimua watu hao, alidai  kuwa watu hao walikuwapo na wamehifadhiwa kwenye chumba maalumu  ili kuwanusuru.
Wakati kukiwa na sintofahamu na ili kuwaondoa watu waliofurika hospitalini hapo, baadaye zilipatikana taarifa kuwa wahusika wa tukio hilo wote wawili wamehifadhiwa kwenye chumba cha maiti kwani wamefariki.
Akizungumza hospitalini hapo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Amani Malima alisema: "Hakuna kitu kama hicho...huu ni uvumi tu. Nani kasema kama kuna hicho kinachoelezwa?" alihoji.
Alisema pia kuwa kutokana na kuwapo kwa hali hiyo,  utendaji kazi wa kawaida katika hospitali hiyo ulilazimika kusimama.   
Nyumba ya wageni
Mwananchi lilifika kwenye nyumba ya wageni iliyotajwa kutokea kwa tukio hilo  iliyopo maeneo ya Tandika, lakini wahusika walikanusha na kusema si 'guest' yao bali ni nyumba nyingine (wanaitaja).
Hata hivyo, Mwananchi lilifika kwenye nyumba hiyo baada ya kuelekezwa kutoka 'guest' ya kwanza, hata hivyo na wao walikanusha kuwapo na tukio hilo.
Wakati tukio hilo likiwa bado kupatiwa suluhu, ilidaiwa jana kuwa mhusika mwenye mke, aliamua kufanya hivyo ili kumnasa mwizi wake na kuelezwa kuwa ili kuwatenganisha, anatakiwa apewe shilingi milioni saba.
Chanzo;mwananchi

No comments:

Post a Comment