Monday, 3 December 2012

Baba haonekani nyumbani, akizaliwa mtoto wa sura tofauti anapiga kelele!


Mpenzi msomaji, leo tujadili jambo lingine baada ya mfululizo wa hoja ya visasi hasa linapotokea tatizo la fumanizi. Bado maoni yanakaribishwa kuhusiana na hilo, lakini wakati tunasubiri, hebu nichombeze jambo lingine ambalo ni tatizo la msingi katika maisha yetu ya kila siku.
Nitalizungumzia katika sura mbili; kwanza pale mtu anapodai mtoto huyu siyo wangu kwa maana hafanani naye na pale mwingine anapohoji mlo huu umetoka wapi pale anapokuwa hajatoa fedha ya matumizi.
Mambo hayo mawili yamekuwa yakizitesa sana familia nyingi na hata kusababisha kusambaratika kwa familia ama kutengana au hata ndoa kuvunjika kabisa.
Naam. Lipo suala la mtoto anazaliwa, kisha baba watoto anakataa eti siyo wa kwake kwa sababu hana sura yake. Hivi majuzi nilisikia jamaa wakibishana juu ya kisa cha mwenzao aliyemfukuza mkewe eti kamzalia mtoto mweupe badala ya mweusi tofauti na watoto wengine.
Jamaa huyo ikaelezwa kuwa alioa ndoa ya nguvu miaka saba iliyopita na wakabahatika kupata watoto wawili ndani ya miaka mitano. Mwaka mmoja uliopita wakabahatika tena kupata mtoto wa tatu. Lakini mtoto huyu kadiri anavyokuwa, anazidi kuwa mweupe wakati wenzake wana weusi wa baba na mama yao. Tena eti pua ni ndefu tofauti na wengine.
Baba kuona hivyo ndipo akaanza kuhoji; “Mbona mtoto anazidi kuwa mweupe wakati sura za wenzake ni weusi? Na hiki kipua nacho vipi?
Mkewe alijitahidi kujitetea, tena aking’ang’ania kuwa anafanana na babu anayemzaa mamake, lakini mume hakukubali na hivyo majuzi kumtimulia kwao hadi jambo hilo lijadiliwe kifamilia. Ndipo jamaa hawa wakawa wanamrushia madongo jamaa kwa hatua hiyo ya kikatili.
Nilipoondoka mahali pale nikawaza: Jamaa analalamika kuwa mtoto hana sura yake, je, yeye alikuwa wapi hadi mtoto azaliwe na sura isiyo yake ndani mwake? Hivi jamaa alikuwa anawajibika ipasavyo kindoa au alikuwa kiruka njia na anapotua nyumbani anakuwa ‘chaka mbaya’? Kama ndivyo, kwanini alalamike wakati ndoa anaibomoa mwenyewe?
Katika mazungumzo ya wale jamaa, mmoja nilimsikia akisema; “Sisi tunamjui ni mchapaji sana huko nje na siyo ajabu akirudi nyumbani kachoka na hatoi huduma stahiki kwa mkewe. Sasa mama huyu atamsubiri asiyemuona hadi lini? Huduma hafifu ndizo kichocheo cha mama kuchepuka nje anapopata uchochoro”. Ama kwa hakika Maisha Ndivyo Yalivyo. Au siyo msomaji wangu?
Suala lingine linalotesa familia zetu, ni ile tabia ya baadhi ya kinababa kuhoji “msosi huu umetoka wapi” wakati hata ndururu(senti) hajaacha kwa ajili ya matumizi.
Tena tabia hii imejiimarisha sana kwa wale ama kipato chao ni cha kubangaiza, au wataafu ambao hawakujiandaa kustaafu na hata pale walipostaafu na kupata mafao yao, wakayatapanya pasipo mpangilio wa kuwekeza ili wajiendeleze kiuchumi. Matokeo yake wanawavuruga hata wake zao ambao wanajitahidi ili maisha yasonge mbele.
Hakuna asiyetambua jitihada za kinamama katika kujiendeleza kiuchumi. Wengi wamejikita katika miradi mbalimbali ya kijasiriamali na hivyo kuwa nguzo muhimu katika pato la familia.
Wapo baadhi ya kinababa ambao wakitoka, wametoka hadi usiku. Haachi hata seti lakini akirudi nyumbani lazima anadai chakula.
Ni vema basi unaporudi na kukuta vimeandaliwa mezani usihoji kwa makeke eti vimetoka wapi? Tena anakuwa mkali wakati hakuacha hela ya matumizi pengine yapata wiki sasa. Je, hii ni haki? Tena haulizi kwa polepole aeleweshwe, anabwatuka nusura ambutue mtu…Ebo!
Katika familia zingine, utakuta baba anao uwezo wa kuacha hela ya matumizi lakini kutokana na kuwa na nyumba ndogo anayoithamini zaidi, huegemea huko na kutojali pale anapoamkia nyumbani kwake. Sasa kwanini mama hata ikiwezekana asikope gengeni au buchani ili mkono uende kinywani?
Na hali hii ya maisha ndiyo inayopelekea kuzaliwa watoto wasiofanana na baba mwenye nyumba. Kumbe mama afanyeje wakati msosi unahitajika nyumbani, baba katimka hakuacha hela ya mboga, akirejea na kukuta mchuzi wa nyama na vikolombwezo vingine atahoji kwa makeke yapi? Tuache utani!

chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment