Thursday, 13 December 2012

Chadema wamng’ang’ania Waziri Magufuli


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtaka Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kueleza kama msimamo alioutoa katika kampeni za Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga ni wa Serikali au wake.Chama hicho kimesema kuwa msimamo alioutoa Magufuli wa kuunga mkono Chama cha ODM ni hatari kwa Tanzania hasa katika uhusiano na nchi hiyo na ni kinyume na mkataba wa kimataifa wa Rome.

Pia kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kueleza kama alimtuma Magufuli katika mkutano huo wa kampeni uliofanyika Desemba 7 mwaka huu, uwanja wa Kasarani na kusema Watanzania wanaunga mkono ODM au la.Msimamo huo wa Chadema ulitolewa jana na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa chama hicho, Ezekieah Wenje.

“Hatujui kama Magufuli alikwenda Kenya kama Serikali au alikuwa amekwenda kama rafiki. Hilo linatupa wasiwasi kwa kuwa hotuba yake ilionekana kama ametumwa na Serikali,” alisema Wenje na kuongeza;

“Alichukua upande katika siasa za Kenya, alimsifia sana Odinga kwamba Tanzania wanampenda wakati kuna mikataba ya kimataifa inayokataza nchi nyingine kuingilia siasa za nchi nyingine kama ilivyoelezwa kwenye Rome Statute.”

Wenje alisema kutokana na hilo ambalo Magufuli amefanya itakuwa mbaya kama mgombea wa chama kingine atashinda nchini Kenya kwa kuwa imeshajionyesha kuwa Tanzania inamuunga mkono Odinga. “Waziri kuchukua upande kwenye siasa za Kenya ni hatari kwa taifa letu na Watanzania wanaishi nchini Kenya.
Itakuwa ni matatizo kwao na hata machafuko yakitokea Tanzania inaweza kuonekana ni chanzo,” alisema Wenje.Alisema ni muhimu Rais Kikwete akaeleza umma kama alimtuma Magufuli Kenya au la ili ujumbe alioutoa ujulikane ni wa nani kwa sababu kama alichokisema ni msimamo wa Serikali basi alitumwa na Rais Kikwete.

Alisema ni muhimu ikajulikana alitumwa na nani kwani taarifa ambazo Chadema inazo ni kwamba CCM hawakualikwa kwenye mkutano huo.“Kama Kenyatta(Uhuru) akishinda humuoni kama italeta shida hapo baadaye? alihoji Wenje.Alisema ni muhimu Serikali ikajua kwamba Rais wa Kenya atachaguliwa na Wakenya wenyewe na si vinginevyo.

Magufuli alipotafutwa kuzungumzia suala hilo hakupatikana kwa simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe ili atoe ufafanuzi hakujibu chochote.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, baada ya simu yake ya mkononi kutoita na taarifa zilizopatikana baadaye kutoka kwa mwandishi wake msaidizi, Irene Bwire, zilieleza kuwa alikuwa kwenye kikao cha baraza la Mawaziri.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape aling’aka akitaka waulizwe ODM ili waeleze walimwalika Magufuli kwa wadhifa upo.“Sikiliza siwezi kuzungumzia suala la ... kama Wenje, kwani itakuwa tunafanya majibizano, we waeleze alipopigiwa Nape alisema waulizwe ODM walimwalika nani,” alisema Nnauye na kuongeza;

Desemba 7 mwaka huu, Magufuli aliungana na Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsavangirai kumpigia debe Odinga, huku akieleza kuwa mwasiasa huyo mkongwe nchini Kenya ndiye anayestahili kuwa Rais wa nchi hiyo.Alisema hakuna sababu zozote za zitakazowafanya Wakenya wasimchague Odinga kwa kuwa ni mcha mungu, hivyo wanatakiwa kujua hilo.
“Nataka kuwaambia Wakenya kwamba Odinga ni mcha Mungu, mnatakiwa kujua hilo. Kama mimi ningekuwa Mkenya ningempigia Odinga kura ili aongoze nchi. Lakini siruhusiwi hata kupiga kura basi nawambia msiache kumchagua huyu atawaongozeni vizuri,”alisema Magufuli.

Magufuli alisema katika wagombea wote waliojitokeza kuwania kiti cha urais nchini Kenya, hakuna anayemfikia Odinga na hiyo inaonyesha kuwa wakimchagua atawasaidia bila ubaguzi.
Alisema na hata Idinga ambaye ni Waziri Mkuu wa Kenya na mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Orange Democratic Party (ODM), ataamua kugombea ubunge katika jimbo lake la Chato, yeye hawezu kumshinda.

“Kwa hiyo nasimama hapa ndugu zangu wana ODM kuwapa pongezi kubwa sana, mmmefanya kitu kikubwa sana kwa sababu mmechagua jembe,” alisema.
Huku akishangiliwa na maelfu ya wajumbe wa mkutano huo, Magufuli alisema kama angekuwa akipiga kura angempa Odinga kura zake zote kwa sababu ni mtu mwenye upendo, uvumilivu, asiye na makuu, sio mbaguzi na anayependa kushirikiana na watu wote.

Aliongeza kuwa Odinga ni mpenda amani na kusisitiza kuwa amelisema hilo kwa sababu amani ni muhimu katika maendeleo ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment