Thursday 13 December 2012

Chagga Day ndani ya Moshi Des. 22


KATIKA kuzikaribisha sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, tamasha la kihistoria la Siku ya Wachaga ‘Chagga Day’ linatarajiwa kufanyika kwenye viwanja vya Ushirika, Moshi Mjini, Kilimanjaro, Desemba 22.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kampuni ya MyWay Entertainment, Paul Mganga, tamasha hilo litakaloanza majira ya saa 4:00 asubuhi, linalenga kuhamasisha jamii juu ya utamaduni wa kabila hilo na mengine, ikiwa ni katika kuenzi mila na tamaduni.
“Vilevile, tamasha hili linahamasisha jamii na familia zao zilizopo ndani na nje ya mikoa yao, kukumbuka nyumbani na kutembelea wazee mara kwa mara.
“Tuna imani kubwa kuwa, zaidi ya watu 3,000 na familia zao, watahudhuria kwa wingi tamasha hili la kihistoria, huku wakipata fursa ya kusikia historia ya kabila la Wachaga kwa kina, kutoka kwa wazee wanaotoka kwenye familia za machifu na Mangi Mkuu wa kabila hilo wanaoishi mkoani Kilimanjaro,” alisema.
Alisema pia kutakuwa na ngoma zote za asili za Kichaga, vikundi tofauti tofauti vya ngoma za asili na sanaa za makabila mengine.
Mganga alisema pia kutakuwa na vyakula vya asili vya aina zote kama kiburu, kisusio, mtori, ndafu, shiro, kiumbo, kitawa, macharari, ngararimo, ng’ande, sambamba na vinywaji vya asili vya kabila hilo kama vile mbege, dadii na vinginevyo.
Alitaja burudani mbalimbali zitakazokuwepo siku hiyo kuwa ni bendi ya Akudo Impact, Mfalme Costa Siboka kutoka Dar es Salaam na wasanii kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, katika tamasha hilo viongozi mbalimbali wa serikali wamealikwa, wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro, viongozi wa asasi zisizo za kiserikali, asasi za serikali, wakurugenzi wa kampuni za utalii na hoteli kubwa za mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Tamasha hilo linadhaminiwa na Safari Lager, Pepsi, Konyagi, Precision Air, Radio 5 FM, Toyo, Samsung, Michuzi Blogspot, Zizou Fashion, Mlonge Bi Makai, Egesha Trading Agency, CXC Africa, Delina Group Enterprises, Linda Media Solution (LIMSO), na Albert Msando Legal Consultant. Kiingilio katika tamasha hilo kimepangwa kuwa sh 5,000.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment