MSANII anayetingisha soko la muziki wa Bongo Fleva kwa sasa, Naseeb Abdul ‘Diamond’, amesema baadhi ya mashairi katika wimbo wake mpya wa ‘Nataka Kulewa’ ametungiwa na Wema Sepetu.
Akizungumza katika kipindi cha Mboni Talk Show, Diamond alisema kutokana na kuimba mambo yanayowagusa wanawake moja kwa moja, kuna mahali Wema alimsaidia kuingiza mashairi kwenye wimbo huo.
Alisema kuna sehemu inaeleza namna mwanamke alivyovikwa pete ya uchumba mbele ya kadamnasi ya watu na baadaye mwanaume kuamua kumuacha bila ya sababu, kitendo ambacho ni kweli alikifanya wakati wa mahusiano yao ya kimapenzi na mrembo huyo.
Hata hivyo, alikanusha tuhuma za kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanamitindo Jokate Mwegelo na Wema huku akidai ni marafiki zake wa karibu ambao kwa namna moja au nyingine wamechangia mafanikio aliyonayo.
“Kwa kweli nitakuwa sina fadhila kama sitawataja wadada hawa, ni kati ya watu watano bora walichochea mafanikio yangu, wakitanguliwa na mama yangu mzazi ambaye ndiye kila kitu kwangu,” alisema.
Aidha, Diamond alisema kwa sasa hana mchumba na atakapompata atautangazia umma ili wamjue.
Mwaka huu msanii huyo alijikuta akitawala katika vichwa vya habari vya magazeti kuhusu mahusiano na warembo hao kwa nyakati tofauti, ikiwemo la kukataa fedha za Wema alizomtunza wakati alipokuwa akitumbuiza katika onesho lake la ‘Diamonds are Forever’ lililofanyika Ukumbi wa Mlimani City.
Pia kuna habari zimeenea mtaani kwamba Wema na Diamond wamerudiana kutokana na kuonekana pamoja katika tafrija mbalimbali ikiwemo ile ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa (birthday) na kwenye tamasha kubwa la muziki la Fiesta ambapo Wema alikuwa akimtambulisha kabla ya kupanda jukwaani.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment