Monday, 17 December 2012

Dk. Bilal awaasa Waislamu kuepuka vurugu.




MAKAMU wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, amewataka Waislamu nchini kufuata kanuni za msingi za Kiislamu, ili kuepuka vurugu, machafuko na uharibifu wa mali kama zilizotokea hivi karibuni.
Dk. Bilal alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana, wakati wa hafla ya kuupokea Mwaka Mpya wa Kiislamu (1434), Hijiriya, iliyoandaliwa na Jumuiya ya Kiislamu ya Istiqama. Alisema utaratibu huo wa Kiislamu ni muhimu, hivyo unapoachwa kufuatwa huweza kusababisha machafuko na kuuana kwa kisingizio cha dini.
Dk. Bilal alisema kanuni za msingi wa Kiislamu ndizo zinazolinda dini hiyo na Waislamu wenyewe pamoja na dunia nzima, huku kanuni hizo zikiwa chanzo cha kujipima na ndizo zinazofanya Uislamu kuitwa Uislamu.
Alisema Uislamu na Waislamu hawana budi kufuata kanuni za msingi, ili wausaidie Uislamu na nchi yao ambapo njia ya msingi ni elimu.
“Kwa mawazo yangu matatizo mengi yanayolenga Uislamu ni ukosefu wa elimu, elimu ya Uislamu wenyewe na elimu nyingine ya dunia,” alisema Dk. Bilal.
Aliongeza kuwa aya za mwanzo alizoshushiwa Mtume Muhammad (SAW), ni kusoma, hakuambiwa kusali au kufunga bali alitakiwa kusoma.
Naye Mwanazuoni Profesa Usamah Ismail Mohamed, aliwausia Waislamu kuwa na tabia njema ambayo inaweza kuwasaidia kufanya wengine wasio Waislamu kuhamia katika dini hiyo.
Kwa upande wake, Sheikh wa Jumuiya hiyo, Juma Nassoro Alhina ameiomba serikali kuifanya siku hiyo kuwa ya mapunziko kila inapofika kama ilivyo katika sikukuu ya miezi ya kawaida (Januari hadi Desemba).
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment