Thursday, 6 December 2012

...FFU mtuhumiwa mauaji ya Mwangosi aendeleza sinema

Matuhumiwa  wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten, mkoani Iringa, Daud Mwangosi, jana alishindwa kufikishwa kortini kutokana na magari ya kubeba mahabusu kukosa mafuta.

Mtuhumiwa huyo, Pasificus Cleophace Simon (23), alitakiwa kufikishwa mahakamani jana  kwa mara nyingine, lakini hatua hiyo ilishindikana baada ya magari ya Jeshi la Magereza ya kubeba mahabusu kukosa mafuta.

Mwendesha Mashtaka, Adolf Maganda, alidai mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Dyness Lyimo, kuwa mtuhumiwa hakufikishwa mahakamani kutokana na tatizo hilo.

Hata hivyo, Maganda hakutoa maelezo zaidi kuhusiana na sababu za magari ya Magereza kukosa mafuta.

Baada ya kudai hivyo, aliiambia mahakama kuwa upelelezi haujakamilika na Hakimu aliiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 19, mwaka huu. 
  
Mtuhumiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Iringa kwa tuhuma ya kumuua mwandishi huyo katika ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi, Mkoa wa Iringa uliofanyika Septemba 2, mwaka huu. 
  
Siku ya kwanza mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa gari la kifahari lenye namba za kiraia T 320 ARC na kwa mara ya pili akifikishwa mahakamani kwa miguu na kuondolewa mahakamani hapo kwa gari namba DFP 2175 pick up akiwa katika ulinzi mkali huku waandishi wa habari wakidhibitiwa na polisi. 

Mmoja wa waandishi wa habari alinusurika kupigwa. 
  
Hii ni mara ya pili kwa mtuhumiwa huyo kutofikishwa mahakamani kutokana na sababu ya magari kukosa mafuta ingawa kipindi hiki hakuna taarifa zozote za kuwapo kwa tatizo ka uhaba wa mafuta.

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliokuwa na silaha na wengine wakivaa kiraia waliweka ulinzi mkali kuhakikisha waandishi wa habari hawapati mwanya wa kupiga picha. 
  
Mwangosi aliuawa kwa bomu Septemba 2, mwaka huu katika kijiji cha Nyololo alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kazi wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chadema. 
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment