Saturday 19 January 2013

Atupa kichanga chooni, asiachwe na mchumba


MKAZI wa Kijiji cha Mnazi, Kata ya Ulumi wilayani Sumbawanga, Prisca Dickson (17), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma ya kutupa mtoto wake chooni mara baada ya kujifungua, kwa hofu ya kuachwa na mchumba wake.
Taarifa zilisema kuwa, mtoto huyo wa siku moja alitupwa katika choo cha jirani, akiwa ameviringishwa kwenye kipande cha kanga.
Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema Prisca alimtupa mtoto huyo mara baada ya kujifungua, na kusababisha kifo chake kutokana na kukosa hewa.
Alisema mwili wa kichanga hicho uligunduliwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mnazi ambao walipita asubuhi katika nyumba hiyo ya jirani, ambapo mmoja wao aliingia kwenye choo hicho kwa lengo la kujisaidia na kukuta maiti hiyo ikielea kisha alitoa taarifa.
Kamanda Mwaruanda alisema baada ya uchunguzi ilibainika kuwa Prisca ndiye aliyefanya kitendo hicho.
“Alipohojiwa na polisi alikiri kuwa ni yeye aliyemtupa mtoto huyo chooni na kuongeza kuwa, alifanya hivyo ili apate kuolewa na mchumba wake waliyepanga kuanza kuishi pamoja katika siku za usoni,” alisema Kamanda Mwaruanda.
Aliongeza kuwa, binti huyo alidai kuwa ilimlazimu kufanya hivyo kwa kuwa, ujauzito aliokuwa nao ni wa mwanaume mwingine.
Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa tukio hilo.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment