Tuesday, 15 January 2013

Mahabusu wa kigeni Keko wagoma


MAHABUSU zaidi ya 50 raia wa kigeni pamoja na Watanzania walioko katika Gereza la Keko jijini Dar es Salaam, wameanza mgomo wa kususia chakula wakishinikiza kesi zao zipangiwe tarehe za kusikilizwa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka gerezani humo, mahabusu hao ni wale wenye kesi za mauaji na dawa za kulevya, ambao wanailalamikia Mahakama Kuu kutowapangia tarehe za kusikilizwa kwa madai kuwa haijapata fedha kutoka serikalini.
Wakizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa majina yao gazetini, baadhi ya mahabusu hao walidai kuwa walioanza mgomo huo jana ni raia 29 kutoka mataifa ya Uingereza, Ireland, Afrika Kusini, Nigeria, Kenya, Uganda, Indonesia, Liberia, Ghana, Iran na Guinea Bissau pamoja na Watanzania 22.
Walisema kuwa wamefikia hatua hiyo kutokana na kesi zao kuendeshwa kwa urasimu wakati wamekaa gerezani humo muda mrefu zaidi ya miaka mitatu hadi mitano bila kusikilizwa.
“Unakuta mtu alikamatwa na dawa za sh milioni kati ya 13 hadi 15, kesi yake inapelekwa Mahakama Kuu wakati hawana fedha, ni kwanini wasingeicha Mahakama ya Kisutu?” walihoji.
Walisema kuwa wako mahabasu wengine wamekaa muda mfupi gerezani humo lakini kesi zao zinaendelea wakati wao wakielezwa kuwa mahakama haina fedha.
“Kilio chetu tuliwahi kumfikishia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa Kanda ya Dar es Salaam, Lukosi, lakini naye alisema fedha hawana. Na jambo baya zaidi ni mkuu wa gereza kutotupa ushirikiano kabisa, maana hata tukimweleza matatizo yetu hataki kutusikiliza,” walidai.
Alipotafutwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angella Kairuki, alisema kuwa suala hilo liko chini ya Idara ya Mahakama, hivyo kushauri kuwa atafutwe Jaji Kiongozi au Msajili wa Mahakama Kuu afafanue.
Hata hivyo juhudi za kuwapata viongozi hao hazikuzaa matunda kutokana na simu zao kutopatikana kwa siku ya jana.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment