Tuesday 15 January 2013

Ulimboka kama Dk. Balali


SAKATA la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, limeanza kuibua taswira mpya kwa umma, kutokana na hatua ya Jeshi la Polisi kukwepa kumhoji wala watu wake wa karibu aliokuwa nao kabla na baada ya kutekwa.
Hata baadhi ya watu aliowatuhumu kwa kuwataja kuhusika na kutekwa kwake nao hawajawahi kuhojiwa.
Na wale waliomwokota katika msitu wa Mabwepande na kumkabidhi katika kituo cha polisi hawajahojiwa. Huku mtuhumiwa pekee Joshua Mulundi akiwa anashinikiza polisi impeleke Dk. Ulimboka amtambue kama alihusika na utekaji huo au la, ili kesi yake iweze kuendelea.
Jana polisi waliibuka na kumwita wakili wake, Nyaronyo Kicheere, afike makao makuu ya jeshi hilo kwa mahojiano leo.
Watu ambao hawajahojiwa ni pamoja na mkazi wa Mabwepande aliyemwokota muda mfupi baada ya kuteswa kwake na Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, aliyekwenda kumchukua mstuni na kumkabidhi polisi.
Wapo pia daktari mwenzake aliyekuwa naye wakati akitekwa na Ramadhani Abeid Ighondu, ambaye Dk. Ulimboka alimtaja kuwa ni mtumishi wa Ikulu, akidai alihusika kumteka.
Ni katika mkorogano kama huo, wadadisi wa masuala ya kijamii wanalifananisha sakata la Dk. Ulimboka na lile la aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Dk. Daudi Balali.
Dk. Balali alihusishwa na tuhuma za ubadhirifu wa mabilioni ya fedha za Akaunti ya Malipo ya Nje ya benki hiyo (EPA), lakini wakati wote hakuwahi kuhojiwa na serikali, kwa kile kilichoelezwa kuwa hawakufahamu alipo hadi baadaye wananchi walipoelezwa kuwa alifariki dunia nchini Marekani.
Kesi za EPA zinaendelea hadi leo kwa baadhi ya wafanyabiashara na vigogo waliodaiwa kuhusika kuchota fedha hizo, ingawa Dk. Balali ambaye alikuwa awe shahidi namba moja inaelezwa kuwa hayupo tena.
Sakata la Dk. Ulimboka nalo linaelekea kuchukua mkondo wa lile la Dk. Balali, kwani kama shahidi namba moja, serikali haitaki kumhoji kupata ukweli wa tukio zima au kuwahoji watu wake wa karibu pamoja na anayetajwa kama mtumishi wa Ikulu ili kuwaondoa hofu wananchi, badala yake wanatafutwa na kuhojiwa watu wa kando.
Wakati wananchi wakihoji alipo Dk. Balali na kutaka arejeshwe nchini, Msemaji wa Rais Ikulu, Salva Rweyemamu, alijibu kwa tambo kuwa serikali ina mkono mrefu, hivyo akihitajika ataletwa nchini.
Ni katika kauli kama hiyo, baadhi ya watu wanahoji kuwa serikali inamaanisha kwamba hata Dk. Ulimboka hahitajiki kwa sasa, ndiyo maana haitaki kumhoji kupata ukweli wa kutekwa kwake.
Lakini katika hatua ya kushangaza, Jeshi la Polisi limemwandikia barua wakili wa wake, likimtaka afike makao makuu leo kwa ajili ya mahojiano akielezwa kuwa ni kwa amri ya polisi chini ya kifungu namba 10(2) na 2(a) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai jalada namba WH/IR/5511/2012..PI Na 5/2012.
Kicheere ndiye alisoma tamko aliloliandika Dk. Ulimboka, Oktaba 17, mwaka jana, kuelezea mkasa mzima uliompata na kuwataja watu aliodai wanahusika katika tukio hilo.
Akizungumza na gazeti hili jana jioni kwa simu, Kicheere alisema kuwa alipokea barua hiyo lakini akawaeleza kwamba leo ana kesi mahakamani asubuhi, hivyo atakwenda kuhojiwa mchana akiwa na wakili wake, Mabere Marando.
“Nimesoma barua yao lakini kwa kumbukumbu zangu sina kosa lolote la jinai kwa mujibu wa jalada hilo, nadhani ni masuala ya Dk. Ulimboka kuhusu tamko lake nililolisoma kwa niaba yake mwaka jana,” alisema.
Alisema kuwa ameona ni vema akajipanga kuongozana na wakili wake pamoja na baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari marafiki zake, kwa ajili ya kumwekea dhamana ikiwa itahitajika.
Alipotafutwa jana jioni kwa simu yake ya kiganjani kuthibitisha kuitwa kwa wakili wa Dk. Ulimboka kwa mahojiano, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, msaidizi wake alisema asingeweza kupatika kwa wakati huo.
Dk. Ulimboka alitekwa, kuteswa na kuumizwa vibaya, ikiwa ni pamoja na kung’olewa kucha na meno usiku wa Julai 26, mwaka jana na kisha kutelekezwa katika msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar e Salaam.
Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam chini ya Kamanda Suleiman Kova, alitangaza kuunda kamati ya wataalamu kutoka ndani ya jeshi hilo ili kuchunguza sakata zima na kuanika ukweli ndani ya muda mfupi.
Hata hivyo tangu kuundwa kwa kamati hiyo, Kova amekuwa akipiga danadana kutoa ripoti akidai amekwisha kuikabidhi kwa wakubwa wake, lakini hivi karibuni Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, alisema hakuna chombo kama hicho na wala Dk. Ulimboka hatahojiwa.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment