Friday 8 March 2013

Madaktari Afrika Kusini waibua madhara zaidi kwa Mhariri Kibanda


Madaktari katika Hospitali ya Millpark, Afrika Kusini wamebaini madhara zaidi aliyopata Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Absalom Kibanda kutokana na unyama aliofanyiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia juzi.

Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, alitekwa, kupigwa na kujeruhiwa vibaya na juzi alasiri alisafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Habari zilizopatikana jana kutoka Afrika Kusini na kuthibitishwa na uongozi wa Tef zinasema madaktari wanaomtibu Kibanda walibaini madhara zaidi ambayo ni pamoja na kukatika kwa mfupa laini (fizi) unaounganisha pua na mdomo pamoja na kulegea kwa meno takriban sita.
Taarifa ya Tef iliyosainiwa na Katibu Mkuu wake, Neville Meena imesema athari hiyo imesababishwa na nguvu na nyenzo walizotumia watesaji kumng’oa meno... “Kutokana na hali hiyo ana maumivu makali sana kwenye kinywa chake.”

Kuhusu meno, Meena alisema hayo sita yaliyoelezwa kwamba yamelegea ni mbali na yale mawili yaliyong’olewa katika tukio la awali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Tef, Kibanda alifanyiwa uchunguzi wa kitabibu na baadaye jana jioni, madaktari walikuwa wakitarajiwa kusoma taarifa ya matokeo ya uchunguzi huo, ili kutafsiri maana ya matokeo yake kisha kutoa mwelekeo wa nini kinafuata au aina ya tiba inayopaswa kutolewa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006), Hussein Bashe alisema madaktari walianza kazi hiyo baada ya Kibanda kufikishwa hospitali hapo juzi usiku.
"Tunashukuru walifika salama, tatizo lilikuwa Uwanja wa Ndege wa Johannesburg, walichelewa kama saa moja hivi kwa masuala ya Uhamiaji, lakini baada ya hapo alipelekwa hospitali.”

“Kwa kuwa alipigwa sindano ya kutuliza maumivu pamoja na usingizi wakati anaondoka, sasa baada ya kuimarika kiakili, alipelekwa chumba cha upasuaji kuangalia jinsi gani ya kulihudumia jicho na hicho kilikuwa kitu cha kwanza na wakati huohuo alianza kufanyiwa uchunguzi ili kujua ameumizwa kiasi gani.”

Katika hatua nyingine, uongozi wa Taasisi iitwayo Southern African Investigative Journalism Forum, jana ulimtembelea Kibanda hospitalini na kueleza masikitiko yake kuhusu yaliyomkuta.

Uongozi huo uliahidi kushirikiana na taasisi za kihabari za Tanzania, kuchunguza tukio hilo kwa lengo la kupata majawabu ya nini kilichojiri na sababu zake.
Leo Tef watakuwa na mkutano wa wahariri wote kujadili hatua zaidi za kuchukua kwa maana mbili; kwanza kuhusu matibabu na afya ya Kibanda na pili usalama wa waandishi wa habari kikazi.

Kibanda alitekwa na watu wasiofahamika ambao walimshambulia  kwa nondo na mapanga na kumng’oa meno mawili, kucha na kumjeruhi jicho la kushoto usiku wa kuamkia juzi.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment