Wednesday 10 April 2013

Askari JWTZ mbaroni wakidaiwa kuua


JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam linawashikilia watu watano wakiwamo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa tuhuma za mauaji ya dereva wa Bajaj, Yohana Cyprian (20).
Watuhumiwa hao ambao majina yao hayakutajwa, wanadaiwa kumuua dereva huyo Aprili 3, mwaka huu, saa 9:00 mchana huko Mbezi Beach kwa Mboma jijini hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa kuuawa kwa Cyprian kuliamsha hasira kwa baadhi ya wananchi.
Alisema kuwa wananchi hao walivamia Kituo cha Polisi Kawe kwa nia ya kumchukua mtuhumiwa aliyedaiwa kuwapeleka wanajeshi hao waliosababisha mauaji.
Kenyela aliongeza kuwa wananchi hao pia walizingira nyumba ya mmoja wa askari mgambo wakitaka kuichoma kwa lengo la kumuua na kulipiza kisasi.
“Baada ya kumuokoa mgambo huyo, wananchi walianza kuwarushia mawe na marungu askari kisha kuchoma matairi barabarani ili wamchukue mtuhumiwa na kumuua.
“Vurugu hizo zilidumu kwa saa mbili ndipo askari wakaamua kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na risasi za baridi wananchi waliokuwa wanafanya vurugu,” alisema.
Kenyela aliwataja askari waliojeruhiwa kuwa ni E1739 D/CPL Alson, D.9054 DCPL Felix na G.5407 PC Azizi aliyepigwa na jiwe kichwani.
Alifafanua kuwa katika vurugu hizo watu 12 walikamatwa na wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
chanzo;daima

No comments:

Post a Comment