Friday 12 April 2013

UVCCM yameguka vipande


MGOGORO ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), unazidi kupamba moto huku mikakati ya kumng’oa Mwenyekiti, Sadifa Juma Khamis na Makamu wake, Mboni Mhita, ikizidi kuanikwa.
Mikakati hiyo inadaiwa kusukwa na kundi moja ndani ya CCM, ikihusishwa na mbio za urais za mwaka 2015.
Uchunguzi wa Tanzania Daima, umebaini kuwapo kwa kundi ambalo Mwenyekiti wa UVCCM, analituhumu kupanga mikakati mbalimbali ya kumng’oa katika nafasi hiyo kwa masilahi binafsi.
Mwanzoni mwa wiki hii, gazeti hili liliripoti kuhusu kundi hilo linalotumia sababu za kuwepo vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa umoja huo uliopita pamoja na madai kwamba mwenyekiti alighushi umri.
Kundi hilo linadaiwa kufadhiliwa na mmoja wa vigogo wa chama hicho wanaotajwa kuusaka urais mwaka 2015 kwa udi na uvumba, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mwenye uhusiano wa karibu na Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete.
Chanzo chetu ndani ya UVCCM kimedokeza kuwa mjumbe huyo ndiye analiwezesha kundi hilo kifedha katika mkakati huo wa kutaka kumng’oa Sadifa kwa vile si miongoni mwa wafuasi wake katika kuelekea mbio za urais za mwaka 2015.

Akizungumza na gazeti hili, Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge, alisema: “Kuna kundi la vijana wapatao kumi kutoka mikoa mbalimbali (majina tunayo), wananifanyia fitina na kuniingilia katika utendaji wangu wa kazi za kila siku kinyume cha katiba ya jumuiya yetu.
“Ninahisi kuwa kundi hili linasaidiwa na mtu mwenye nguvu au mwenye mamlaka kwenye chama. Nasema hivyo kwa sababu sasa hii ni mara ya tatu,” alisema.
Sadifa alisema kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi wao uliofanyika mjini Dodoma, watu hao walikuja na mabango kwenye mapokezi yake jijini Dar es Salaam ofisi ndogo za chama Lumumba.
Alisema kuwa kundi hilo liliandaa watu wakafanya fujo hadi kupigana, na kufikia hatua ya kutosalimiana sasa.
“Nimefika makao makuu juzi, nikakuta vijana watatu waliokuwepo hapo nikawasalimia, lakini mwingine alitaka kunishambulia nikakimbilia ofisini kwa Nape Nnauye,” alisema.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutotajwa majina yao, baadhi ya wajumbe wa baraza hilo walisema: “UVCCM kuna tatizo tena kubwa.” Kwamba kilichotokea na kinachotokea sasa ni mwenyekiti wao kushindwa kujibu hoja.
“Tulihoji utaratibu aliotumia katika uteuzi wa makatibu kwenye jumuiya yetu, akasema sisi tunataka kuchanganya mapenzi na kazi, kitu kilichozua malumbano katika kikao chetu,” walisema.
Walidai kuwa kauli hiyo iliwaudhi na sasa hata kama hawana mpango wa kumwondoa madarakani, atajiondoa mwenyewe kwa kushindwa kusimamia yale ambayo aliahidi.
“Mwenyekiti wetu ni tatizo,” alisema mmoja wa wajumbe wa UVCCM huku akionesha ujumbe mfupi wa simu ambao amewahi kutumiwa na mwenyekiti huyo.
Ujumbe huo ulisomeka: “Usinitumie sms za kipumbavu, wananena respect yourself, if you can not respect yourself no body will respect you… ukianza nitamaliza.”
Mjumbe huyo aliongeza kuwa, Sadifa alishinda kwa rushwa, kwamba kila mjumbe alipewa kati ya sh 50,000 hadi 100,000 ili kufanikisha uchaguzi.
“Mwenyekiti wa chama alikuja akaonya kuhusu rushwa, lakini alipotoka tu, miguu yake ikafutwa kwa kugawiwa sh 20,000 za haraka haraka kwa kila mjumbe,” alisema.
Alipotafutwa mmoja wa wajumbe wa kundi linalotuhumiwa na mwenyekiti, alisema: “UVCCM ni mbovu yote, si suala la taasisi, huu ndio msimamo wangu”.
“Mimi baada ya uchaguzi nilisimama ukumbini na niliwaambia wajumbe kuwa kama kuna mtoto wa mnyonge au maskini aliyepokea rushwa ili kupiga kura, atakuwa amepanda mbegu na kizazi chake kitavuna. Heri kuanguka kwa heshima kuliko kushinda kwa fedheha,” alisema.
Alisema kuwa mwenyekiti wao ambaye kwa sasa anawatuhumu kwenye vyombo vya habari anakosea. Kwamba hana haja ya kupiga kelele za rushwa, vijana wamesaini wazi kumshtaki kuwa alishinda kwa rushwa.
“Mimi tangu uchaguzi wetu umalizike sijaongea, nakwambia siku nikiongea hata ardhi itajua,” alisema.
Wajumbe wengine waliohusishwa na mkakati wa kumng’oa mwenyekiti walikuwa wakali kila walipopigiwa simu na hata kufikia hatua ya kuzikata.
Katibu wa UVCCM, Martine Shigela, alisema jumuiya hiyo ipo imara, hakuna tatizo na kwamba wiki ijayo watakaa na kamati ya utekelezaji.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment