Friday, 5 July 2013

HABARI YA KUSIKITISHA:Mghana alivyouawa kinyama Bagamoyo


Dar es Salaam. Salimu Mohamed Marwa (25) ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa magari, raia wa Ghana, Jose ph Opong.
Mbali na Marwa, ambaye amesoma kozi ya urubani, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Peter Charles Mayalla, ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo.
Washtakiwa hawa hao, ambao wote ni wakazi wa Bagamoyo mkoani Pwani wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inayosikilizwa na Jaji Njengafibili Mwaikugile.
Wanadaiwa kuwa Septemba 10, 2010, walimuua kwa makusudi Opong, kwa kumkatakata sehemu mbalimbali za mwili, baada ya kumlewesha kwa dawa za kulevya na kisha kwenda kumzika katika msitu wa Kaole.
Awali Marwa, alitiwa mbaroni kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, baada kukamatwa akiwa na nyaraka za magari ya marehemu Opong katika harakati za kuyauza magari hayo yaliyokuwa Bandarini.
Alikamatwa baada ya mke wa marehemu Opong kutoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi, Septemba 22, kuwa mumewe alikuwa hajaonekana tangu Septemba 9, na kwamba aliondoka kwenda kushughulikia magari yake yaliyokuwa bandarini.
Baada ya taarifa hizo, Polisi walitoa taarifa bandarini kuwa mtu yeyote atakayefika kutaka kutoa magari hayo asiruhusiwe, na Septemba 28, ndipo Salim alipokamatwa akiwa na nyaraka za magari hayo, mkataba wa mauziano na kitambulisho cha marehemu Opong.
Kwanza alipoulizwa kuhusu mahali alipozipata nyaraka hizo alisema kuwa ameuziwa na Joseph Opong, lakini alipoulizwa mahali alikokuwa Opong alijibu kuwa hajui na kwamba baada ya kuuziana, waliachana.
Kuhusu kitambulisho ambacho kilikuwa na jina la Opong lakini kikiwa na picha yake, alishindwa kueleza lolote.
Hivyo kesho yake Septemba 29, timu ya Upelelezi kutoka Polisi Kanda ya Dar es Salaam ikiongozwa na Inspekta (Mkaguzi wa Polisi), Saidi Mohamed Mwagara ilikwenda na mtuhumiwa nyumbani kwake Bagamoyo, kufanya ukaguzi ambao ungewezesha kubaini alikokuwa Opong.
Inspekta Mwagara alidai kuwa hata hivyo katika ukaguzi wao hawakuweza kupata kielelezo chochote cha kuwasaidia, na kwamba wakati wakiwa kwa mtuhumiwa huyo, alimtaka mtuhumiwa awaeleze ukweli kwa kuwa walikuwa wameshachoka.
Alidai kuwa mshtakiwa huyo alisema naye ameshachoka kuzunguka na kwamba sasa anataka awaeleze ukweli, na ndipo akasema kuwa Opong tayari wameshamuua, na kwamba yuko tayari kwenda kuwaonyesha walikomzika.
Aliongeza kuwa kutokana na maelezo hayo kwa kuwa ilikuwa jioni, waliondoka na kwenda katika Kituo cha Polisi Bagamoyo ambapo mshtakiwa aliwaelezea kuhusu tukio hilo na kwamba baadaye usiku aliwapeleka katika Msitu wa Kaole na kuwaonyesha mahali walikokuwa wamemzika Opong.
Inspekta Mwagara aliendelea kudai kuwa waliweka alama katika eneo hilo na kwamba waliweza hata kupata mapanga mawili yaliyotumika kumuulia Opong, kisha wakarudi kituoni.
Alidai kuwa kutokana na maelezo hayo ya mshtakiwa walitoa taarifa kwa viongozi wake kisha wakaomba kibali kutoka kwa Korona (Hakimu wa Wilaya) wakaenda kufukua mahali pale Marwa alipowaonyesha kuwa ndipo walipomzika Opong.
Aliongeza kuwa walipochimba mahali hapo kweli walikuta mwili wa mtu ukiwa ndani ya mfuko mkubwa wa kubebea nguo wenye zipu.
Aliendelea kuwa waliifungua zipu ile wakakuta mwili wa mtu ukiwa umekunjwakunjwa huku ukiwa umekatwakatwa sehemu mbalimbali za mwili, ukiwa umeshaharibika, kisha wakaupeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa uchunguzi ndipo ukatambulika kuwa ni wa Opong.
Baada ya tukio hilo alimwagiza Ditektvu Koplo Elia aandike maelezo ya onyo ya mshtakiwa, ambayo mahakama imeyapokea kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Katika maelezo hayo ambayo yalisomwa mahakamani hapo, mshtakiwa Marwa alieleza namna alivyokutana na kufahamiana na Opong, njama na mipango ya kumuua, lengo la kumuua na jinsi walivyofanikiwa kutekeleza mauaji hayo.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, Septemba 2, 2010, saa 15.00, mshtakiwa huyo akiwa na rafiki zake Sudi na Abdallah, wakitokea Mwenge wakienda kuuza madini yao, walikutana na mtu ambaye hakuwa akimjua, eneo la Kinondoni Moroko jijini Dar es Salaam.
Mtu huyo alimuuliza mshtakiwa Marwa kwa Kiingereza kama anajua kuongea Kiingereza naye akamjibu kuwa anajua .
Mtu huyo alijitambulisha kuwa anaitwa Joseph Opong na kwamba alikuwa anataka kwenda Bagamoyo lakini alikuwa amesahau kituo cha mabasi ya kwenda huko kwa kuwa alikuwa na muda mrefu tangu alipotoka huko kwa mara ya mwisho.
Mshtakiwa Marwa alimwambia Opong kuwa asiwe na wasiwasi amefika kwa kuwa na yeye ni mkazi wa Bagamoyo. Hivyo alimuuliza kuwa alitaka kwenda kumwona nani na Opong akamjibu kuwa kuna ndugu yake ambaye ni maarufu kwa jina la Mghana.
Mshtakiwa Marwa alisema kuwa alimwambia Opong kuwa anamjua Mghana kwa kuwa anakaa naye jirani na kwamba kutoka kwake hadi kwa ndugu yake huyo ni nyumba ya tatu tu.
Hivyo Opong alimwomba namba ya simu ya huyo ndugu yake, lakini yeye mshtakiwa Marwa akamwambia kuwa hakuwa nayo ila alikuwa na namba ya mtoto wake, Issa.
Itaendelea kesho
Hata hivyo mshtakiwa Marwa alipompigia simu Issa, hakumpata, ndipo akampigia mtoto mwingine wa ndugu wa Opong ambaye alimpata na kumwambia kuwa amekutana na ndugu yake Dar es Salaam angependa kuzungumza na baba yake.
Mtoto huyo wa ndugu yake Opong alimtumia namba ya simu ya baba yake na Opong akampigia ambapo wakaongea na Opong akamwambia kuwa ana magari yake bandarini anataka kuyauza.
Opong alimwomba ndugu yake huyo amsaidie kumpata mtu wa kuyatoa au mtu wa kuyanunua, lakini nduguye akamwambia kuwa asiende Bagamoyo bali yeye angemfuata Dar es Salaam.
Kabla ya kuachana, Opong alimwonyesha mshtakiwa Marwa nyaraka za magari hayo matano yaliyokuwa bandarini kisha wakapeana namba za simu hatimaye wakaagana wao wakaenda kuuza madini yao.
Mshtakiwa Marwa na wenzake waliporudi Bagamoyo walikutana na Nurdin, rafiki wa Sudi, ambaye waliongozana naye wote hadi nyumbani kwake (Marwa), ambako waliongea sana.
Baadaye Sudi na Abdallah waliondoka, lakini Nurdin ambaye pia ni mkazi wa Bagamoyo alibaki na akala kwa mshtakiwa Marwa na asubuhi ya Septemba 3, 2010 aliondoka kwenda Dar es Salaam.
Baadaye, mchana wa siku hiyo mshtakiwa Marwa alikwenda kwa Sudi akamkuta Nurdin na wakiwa hapo Opong alimpigia simu mshtakiwa Marwa akimweleza kuwa alikuwa hajaonana na ndugu yake.
Mshtakiwa Marwa alimwambia Opong kuwa yeye ana jamaa yake anaitwa Nurdin anataka gari ya Vicks, na akamshauri Opong aende Bagamoyo aongee na Nurdin wafanye biashara.
Jioni ya siku hiyo, Opong alikwenda Bagamoyo mshtakiwa Marwa akampokea kisha akampeleka kwa nduguye (Mghana).
Baada ya mzungumzo kati ya Opong na ndugu yake huyo, waliondoka tena wote na kurudi nyumbani kwake kwa mshtakiwa Marwa, ambapo waliendelea kunywa bia.
Baadaye usiku huohuo, mshtakiwa Marwa alimpigia simu Nurdini kumweleza kuwa Opong ameshafika. Nurdin alimuuliza kama ana fedha, na yeye akamjibu kuwa kama ana magari ni lazima atakuwa nazo.
Nurdini alimwambia mshtakiwa Marwa kuwa afanye mchongo ili wakapate fedha. Mshtakiwa Marwa alimuuliza Nurdin kuwa ni mchongo gani huo na Nurdin akasema kwa kuwa Opong si Mtanzania basi watawatafuta askari Polisi wamkamate.
Nurdin alisema kuwa kwa njia hiyo wataweza kupata fedha kutoka kwa Opong.
Hivyo Nurdin aliwasiliana na askari Mwamba ambaye alifika nyumbani kwa mshtakiwa Marwa akiwa na mwenzake wakadai anamtaka mgeni Mghana aliyemo ndani humo kwa kuwa ana dawa za kulevya.
Opong aliposikia hivyo alipiga kelele sana kiasi kwamba hata askari wale walishindwa kumfunga pingu wakaamua kuondoka zao, na mshtakiwa Marwa alijitahidi kumtuliza Opong hadi akatulia na hatimaye akalala.
Kesho yake Septemba 4, asubuhi walikwenda kwa Nurdin ambapo mshtakiwa Marwa alimtambulisha Opong kwa Nurdin kuwa ndiye anataka gari. Walizungumza na wakakubaliana wakaenda wote watatu bandarini Dar es Salaam kuangalia hayo magari.
Baada ya kuyaona magari hayo, Opong aliwapa nakala za nyaraka za magari hayo kisha wakaagana kwa makubaliano kwamba wakiwa tayari watampigia simu.
Jioni Nurdin alimpigia simu mshtakiwa Marwa akimwambia kuwa ni kwa nini wasimleweshe Opong ili waweze kuchukua magari yote yale, lakini Marwa alipinga kuwa Opong akizinduka atajua kuwa ni yeye alimfanyia hivyo.
Hivyo walikubaliana kuwa ni bora wamuue huku Nurdin akitamba kwamba hizo ndiyo kazi zake na kwamba ameshazifanya nyingi tu.
Kesho yake, Septemba 5, Nurdni alimpigia simu Marwa akimtaka amtafute Opong, huku akisema ameshaandaa vijana wa kazi.
Septemba 6, Nurdin alimwambia Marwa kuwa amepata wazo la kumchanganyia Opong dawa za kulevya katika kinywaji, na Septemba 7, Nurdin alikwenda kwa Marwa akamwambia kuwa ana dawa ya bei mbaya kwani alikuwa ameinunua kwa Sh70,000.
Marwa aliifanyia majaribio dawa hiyo akalewa kiasi cha kukosa fahamu na akazinduka kesho yake, Septemba 8. Baada ya kuzinduka alimpigia simu Opong aende Bagamoyo kesho yake, Septemba 9, akimwambia kuwa fedha iko tayari na akamwelekeza kwa mama yake Mlingotini.
Asubuhi ya siku hiyo, Septemba 9, Marwa alienda kwa mama yake Mlingotini kula sikukuu, na mama yeye alikwenda Mugumu kwenye mahafali ya shule yake.
Jioni Nurdini alimtaka Marwa ampigie simu Issa Abdallah naye akafanya hivyo. Abdallah alifika kwa mama yake Marwa saa 11 akamkuta Opong tayari ameshafika.
Waliondoka wote wakaenda Hoteli ya Boma kula na kunywa, na wakati wakiendelea, Marwa alimvizia Opong, akamwekea dawa kwenye glasi yake.
Baadaye Opong alienda chooni, na Marwa akapata tena nafasi nzuri ya kumwekea dawa kwenye glasi yake ya pombe. Opong aliporudi aliendelea kunywa na baadaye akalewa sana hadi akashindwa kujitambua.
Walimchukua hadi nyumbani kwa mama yake Marwa, wakamweka katika chumba akalala, na saa moja usiku Marwa aliampigia simu Nurdini akamweleza kuwa tayari Opong kalala.
Hivyo saa 3 usiku, Nurdin alifika na gari aina ya Toyota Mark II nyeusi ikiendeshwa na mtu mwingine. Marwa na Issa walimtoa Opong nje kupitia mlango wa nyuma hadi kwenye gari wakamuweka kwenye kiti cha mbele wao wakakaa nyuma.
Waliondoka naye hadi nyumbani kwa Marwa ambako walimkuta Mayala (mshtakiwa wa pili) ndani akiwa bado hajalala. Nurdin alimtaka Mayala aondoke ili Opong alale.
Issa hakujua kuwa walitaka kumuua ila alidhani ni kumlewesha tu ili wamwibie nyaraka zake, hivyo yeye aliondoka saa tano, akawaacha Marwa, Nurdin na Mayala.
Baada ya Issa kuondoka, Nurdin na Mayala walichukua mapanga mapya ambayo Mayala alikuwa ameyanunua kwa fedha aliyopewa na Marwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Walimshusha Opong kutoka kitandani na kumweka chini. Nurdin akamkata panga la shingoni na usoni. Baada ya Nurdin kukata shingoni, Opong alikoroma sana. Hivyo Marwa alichukua nguo akamziba mdomoni ili watu wasiweze kusikia alivyokuwa akikoroma.
Alipofariki walimhifadhi ndani humo hadi Septemba 10. Nurdini alikwenda kutafuta mfuko wa zipu wa kumhifadhia kisha akaleta lile gari walilolitumia awali, wakati huo akiwa analiendesha mwenyewe.
Waliukunja mwili wa Opong kama nguo na kuuweka kwenye huo mfuko kisha wakambeba na kumweka kwenye buti ya gari. Marwa alichukua jembe la mama wa nyumba yake ambalo lilikuwa nje, kisha wakaendesha mpaka Mbegani
Nurdini alisimamisha gari akaenda kuchukua jembe lingine nyumba ya jirani kisha wakaendelea mbele zaidi, ndani ya Msitu wa Kaole wakachimba shimo na kuufukia humo mwili wa Opong.
Walirudi nyumbani na Marwa akachukua nguo za marehemu Opong zilizokuwa na damu akazitupa kwenye shimo la choo, na mapanga yote Mayala aliyatupa alikojua yeye.
Kisha alifanya usafi wa damu chumbani na simu zote za Joseph (Opong) alikuwa nazo yeye Mayala.
Baadaye waliwatafuta wanunuzi wa magari yale ambao walienda kuyaona na wakawapa nyaraka zote, wakawapatia fedha Dola za Marekani 3900 ambazo waligawana.
Katika fedha hizo, zilibakia Dola 1000 ambazo ndizo zilizosababisha Marwa akatiwa mbaroni wakati akizifuatilia.
Marwa alihitimisha maelezo yake hayo kwa kusema: “Haya ndiyo maelezo yangu niliyoyatoa mbele ya dada yangu Farida Said Namchumbe , nikiwa na akili timamu na kwa hiyari yangu bila vitisho.
Nathibitisha kuwa maelezo haya ni sahihi kadri ya ufahamu wangu, bila vitisho bali kwa hiyari yangu.”
Marwa alisaini maelezo hayo akaweka na alama ya dole gumba na dada yake Farida pia alisaini kuthibitisha kuwa maelezo hayo yametolewa na mshtakiwa Marwa mbele yake kwa hiyari yake bila kushurutishwa.
Mahakama Kuu baada ya kupokea na kusikiliza maelezo hayo ya mshtakiwa, Jaji Mwaikugile aliahirisha hadi kikao cha mahakama kijacho kwa tarehe itakayopangwa na msajili.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment