Tuesday, 9 July 2013

Kesi ya ugaidi sarakasi tupu

HATIMA ya kesi ya ugaidi inayowakabili makada watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), sasa ipo mikononi mwa Mahakama Kuu baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora ilikofunguliwa kusema haina uwezo wa kusikiliza kesi ya ugaidi.
Wakati Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Tabora, Issa Magoli, akiisukumia Mahakama Kuu kesi hiyo, wakili wa watuhumiwa hao, Peter Kibatala, aliliambia Tanzania Daima kuwa wameshafanya utaratibu wa kupeleka shauri lao Mahakama Kuu baada ya kupewa nakala ya uamuzi huo.
Makada hao wa CHADEMA wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi ni Katibu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo, Evodius Justinian, Oscar Kaijage , Seif Kabuta na Rajab Daniel, wanaotuhumiwa kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha, katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga mwaka 2011.
Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Magoli alisema mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza kesi hiyo, hivyo akaiahirisha kesi hiyo hadi Julai 22, mwaka huu.

Hakimu Magoli kabla ya kuahirisha shauri hilo aliwashauri mawakili wa upande wa utetezi wawasilishe hoja zao Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo watapatiwa ufumbuzi wa kisheria.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili, wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala, saa chache baada ya uamuzi huo, alisema wameshapeleka Mahakama Kuu Kanda ya Tabora maombi kwa hati ya dharura ya kutaka iipitie upya kesi hiyo ya ugaidi.
Aliongeza kuwa maombi hayo yamepokewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na wanasubiri kupangiwa tarehe nyingine na Mahakama Kuu ili kesi hiyo isikilizwe.
Alisema katika maombi yao wameomba Mahakama Kuu ipitie shauri hilo, pia kuona kama ni halali kisheria kwa washtakiwa hao kufunguliwa kesi hiyo baada ya awali watuhumiwa wanne (isipokuwa Kilewo), mashtaka yao yaliondolewa na kisha kukamatwa na kufunguliwa mashitaka mapya.
Kwa mara ya kwanza watuhumiwa hao walisomewa shitaka la ugaidi Juni 24, mwaka huu, wakidaiwa walimteka na kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha, katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011.
Awali kabla ya kusomewa shitaka la ugaidi ambalo kwa sasa mahakama inasema haina uwezo wa kusikiliza, mwanzoni walifunguliwa shitaka la kushambulia na kudhuru mwili, ambapo Mahakama ya Wilaya ya Igunga iliwaona hawana hatia, hivyo kuwaachia huru lakini walikamatwa tena.
Kesi hiyo ilisikilizwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora mjini. Jocktan Rushwera, ndiye aliyesikiliza hoja za mawakili wa utetezi, waliomtaka kuifuta kesi hiyo. Hata hivyo haijulikani kwanini kesi ilisikilizwa halafu baada ya kubadilisha hakimu, kwa kesi hiyo hiyo mwingine akasema mahakama hiyo haina uwezo wa kuisikiliza.
Upande wa serikali uliwakilishwa na Wakili Juma Massanja na Ildefons Mukandara.
Awali watuhumiwa hao waliposomewa shitaka, jopo la mawakili wa utetezi, Abdalah Safari na Peter Kibatala, liliomba mahakama hiyo iyafute mashitaka hayo kwa sababu ya kutokuwa na uhai.
Mawakili hao wa utetezi walidai kuwa mashitaka hayo hayana uhai kwa sababu yamefunguliwa bila ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Pia mawakili hao walidai kuwa sheria za uendeshaji wa makosa kama hayo hapa nchini zinadai kuwa mashitaka kama hayo yanapofunguliwa ni lazima ridhaa ya DPP iwepo, lakini ridhaa hiyo haipo, hivyo yatupwe.
Waliongeza sababu ya pili kuwa maelezo hayaoneshi kosa husika ni la kigaidi, tofauti na makosa mengine ya kawaida kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hivyo waliomba yafutwe au yafunguliwe kama kosa la kawaida.
Upande huo wa utetezi pia ulidai kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, inaelekeza kuwa mshitakiwa ashitakiwe katika mahakama yenye mamlaka na hadhi kama ile waliyopelekwa katika maeneo yale walikokamatwa.
Hivyo mawakili waliiomba mahakama itupilie mbali shitaka, kwani washitakiwa kama walikuwa na hatia walipaswa kushitakiwa katika maeneo yao walipokamatwa.
Upelelezi wa Lwakatare bado
Wakati huo huo, mkoani Dar es Salaam, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha kesi ya kula njama na kutaka kumuua kwa sumu Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis Msacky, inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.
Hakimu Mkazi, Alocye, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 22, mwaka huu kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.
Awali, Wakili Mkuu wa Serikali, Ponsia Lukosi, aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Lwakatare yupo nje kwa dhamana, Ludovick bado yupo gerezani baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika kisheria ambapo kila mdhamini atatakiwa asaini bondi ya sh milioni 10 pamoja na washitakiwa wenyewe.
Pia mshitakiwa anatakiwa kusalimisha hati yake ya kusafiria mahakamani na kutotoka nje ya Jiji la Dar es Salaam bila ya kibali cha mahakama.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment